Tanzania imetumia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela 2026 kusisitiza dhamira yake ya kuendeleza amani, umoja wa kitaifa, maridhiano na maendeleo jumuishi, huku ikiweka mkazo katika kuwawezesha vijana kama nguzo ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika tarehe 18 Julai, 2026 katika Ofisi za WEEDO Tanzania jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Bw. Charles Ngeleja Kadonya, alisema maadili ya Hayati Nelson Mandela yanaendelea kuwa dira ya kujenga taifa lenye mshikamano na maendeleo endelevu.

Bw. Kadonya alisema Tanzania inaendeleza urithi huo kwa kuwekeza katika elimu bora, ujuzi, ubunifu, ujasiriamali na matumizi sahihi ya teknolojia ili kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa. Alisisitiza kuwa uongozi bora hujengwa kwa mazungumzo, maridhiano na kuheshimiana.

Kwa upande wake, Kaimu Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Ronald Tran Ba Huy, alihimiza jamii kuenzi Siku ya Mandela kwa kujitolea dakika 67 kama ishara ya miaka 67 ya huduma ya Mandela katika kutetea haki za binadamu, usawa na ustawi wa jamii.

Naye Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Mhe. Noluthando Mayende-Malepe, alisema hayati Nelson Mandela atakumbukwa kama kiongozi aliyesimamia uvumilivu, maridhiano, utawala bora na amani. Aliongeza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania, Umoja wa Mataifa na wadau wa maendeleo utaendelea kuimarisha usawa wa kijinsia na fursa kwa vijana.

Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela huadhimishwa kila tarehe 18 Julai kwa lengo la kuenzi mchango wake katika mapambano ya haki za binadamu, usawa na uhuru, huku ikihamasisha watu duniani kushiriki katika matendo ya kujitolea na huruma kwa ajili ya kuboresha maisha ya wengine.