Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS), Mhe. Moussa Saleh Batraki, amewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku nane kuanzia Julai 19 hadi 26, 2026, ikiwa ni ziara yake ya kwanza nchini tangu alipoanza kutekeleza majukumu hayo mwezi Machi 2025.
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Mhe. Batraki alipokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Mkuu wa Ujumbe wa Tanzania katika Umoja wa Ulaya, Mhe. Jestus Nyamanga, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Ellen Maduhu, pamoja na maafisa wengine kutoka Wizara hiyo.
Akiwa nchini, Katibu Mkuu huyo anatarajiwa kufanya mazungumzo ya ngazi ya juu na viongozi wa Serikali jijini Dar es Salaam na Zanzibar, ikiwa ni pamoja na kukutana na Wabunge na Mawaziri wenye dhamana ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mifugo na Uvuvi, pamoja na Uchumi wa Buluu.
Aidha, Mhe. Batraki anatarajiwa kutembelea miradi mbalimbali ya Uchumi wa Buluu ili kujionea kwa karibu juhudi za Tanzania katika usimamizi endelevu wa rasilimali za bahari, maendeleo ya sekta ya uvuvi na kukuza uchumi wa maeneo ya pwani.
Katika mazungumzo yake na viongozi wa Serikali, pande hizo mbili zinatarajiwa kujadili namna ya kuendeleza ushirikiano kupitia utekelezaji wa miradi ya vitendo, pamoja na kuhamasisha upatikanaji wa fedha, teknolojia na utaalamu kwa ajili ya maendeleo ya Uchumi wa Buluu.
Ziara hiyo pia inatarajiwa kuimarisha nafasi ya Tanzania ndani ya OACPS na kuendeleza ushirikiano wa kimataifa katika maendeleo endelevu na matumizi bora ya rasilimali za bahari.
OACPS ni jukwaa linalojumuisha nchi wanachama 79 kutoka Afrika, Karibiani na Pasifiki. Jukwaa hilo linasimamia na kuratibu ushirikiano, ukiwemo wa kiuchumi na kibiashara, kati ya wanachama wake na Umoja wa Ulaya kupitia Mkataba wa Samoa.

