New York, Marekani

Spika wa Bunge Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu (Mb) amesema Bunge la Tanzania limechukua hatua madhubuti za kuhimiza matumizi ya magari ya umeme pamoja na gesi.

Amesema hatua hizo zimelenga kuimarisha utekelezaji wa mipango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

 

Mheshimiwa Spika ameyasema hayo leo Julai 14, 2026 wakati akiwasilisha taarifa ya Bunge la Tanzania kuhusu matumizi ya Nishati Safi kwenye Jukwaa la Kibunge katika Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu (HLPF) 2026.

 

Mkutano huo umefanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN), jijini New York, nchini Marekani.

 

Amesema Bunge la Tanzania limepitisha marekebisho ya sera na sheria za kodi yaliyopunguza ushuru wa magari ya umeme kutoka asilimia 25 hadi asilimia 10 na kwamba misamaha mbalimbali ya ushuru na kodi kwa baadhi ya magari yanayotumia umeme na gesi imetolewa ili kuongeza matumizi ya usafiri rafiki kwa mazingira.

 

“Hatua hizi zinalenga kuwahamasisha wananchi kutumia magari ya umeme na yanayotumia gesi, kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa, kupunguza utegemezi wa uagizaji wa mafuta ya petroli kutoka nje ya nchi na kulinda mazingira,” alisema Mheshimiwa Zungu

 

Aidha, amesema Tanzania imeendelea kuimarisha mifumo ya kitaasisi ya kushughulikia masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwa kuanzisha vitengo maalumu vya usimamizi wa masuala hayo, kuimarisha uhifadhi wa vyanzo vya maji na kuweka mfumo wa kitaifa wa ufuatiliaji wa kaboni.

 

“Hatua hizi zinaonesha dhamira ya Tanzania ya kujenga uchumi unaozingatia maendeleo endelevu huku ikichangia juhudi za dunia za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,” amesema.

 

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Zungu ameialika Jumuiya ya Kimataifa kushiriki Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) utakaofanyika jijini Arusha, akisisitiza kuwa Tanzania ni nchi salama na ipo tayari kuwakaribisha wajumbe kutoka mataifa mbalimbali.

“Ninawakaribisha nyote Tanzania kushiriki Mkutano wa 153 wa IPU jijini Arusha. Hakuna changamoto za kiafya zinazopaswa kuwapa wasiwasi wageni wanaokuja Afrika Mashariki, hususan Tanzania, karibuni mfurahie Mlima Kilimanjaro na visiwa vya marashi ya karafuu, Zanzibar,” alisema Mheshimiwa Zungu.