* Mhandisi Samaje azindua Ukumbi wa Mikutano wa Prof. Abdulkarim Mruma

* Watumishi GST watakiwa kuzingatia maadili, ubunifu na utoaji wa huduma bora

Dodoma

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Mhandisi Ally Samaje, amesema taasisi hiyo katika mwaka wa fedha 2026/27 itaendelea kuimarisha utafiti wa madini na kuboresha huduma za maabara ili kuongeza ufanisi katika sekta ya madini na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Mhandisi Samaje amesema hayo leo Julai 15, 2026, wakati akifungua kikao cha watumishi wa GST kilicholenga kupitia utekelezaji wa majukumu kwa mwaka wa fedha 2025/26 na kujadili vipaumbele vya mwaka wa fedha 2026/27, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Prof. Abdulkarim Mruma, jijini Dodoma.

Katika kikao hicho, Mhandisi Samaje amewataka watumishi wa GST kuzingatia maadili ya kazi, ubunifu na ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao ili kuhakikisha wananchi na wadau wa sekta ya madini wanapata huduma bora, zenye ubora na kwa gharama nafuu.

Amesisitiza kuwa maadili ya kazi ni msingi wa utoaji wa huduma bora, huku ubunifu ukiwa kichocheo cha kuongeza ufanisi wa taasisi. Aidha, amewahimiza watumishi kuendelea kuimarisha utamaduni wa kufanya kazi kwa ushirikiano (teamwork), akieleza kuwa mshikamano ni nguzo muhimu katika kufanikisha malengo ya GST.

Akizungumzia kuanzishwa kwa Mfuko wa Tafiti za Madini, Mhandisi Samaje ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutengwa kwa asilimia 10 ya mapato yatokanayo na sekta ya madini kwa ajili ya kugharamia shughuli za utafiti wa madini nchini.

Amesema hatua hiyo itaongeza uwezo wa GST kufanya tafiti za kina, kubaini maeneo mapya yenye rasilimali madini, kuboresha taarifa za kijiolojia na kuimarisha huduma za maabara kwa manufaa ya sekta ya madini na Taifa kwa ujumla. Aidha, amewataka watumishi kujiandaa kutekeleza jukumu hilo kwa weledi, uwajibikaji na uadilifu ili kuhakikisha fedha hizo zinaleta matokeo yaliyokusudiwa.

Kabla ya kuanza kwa kikao hicho, Mhandisi Samaje alizindua rasmi Ukumbi wa Mikutano wa Prof. Abdulkarim Mruma baada ya kukamilika kwa ukarabati wake. Ukumbi huo unatarajiwa kutumika kwa mikutano, makongamano na shughuli nyingine rasmi za taasisi.

Katika kikao hicho, wakurugenzi na wakuu wa vitengo waliwasilisha taarifa za utekelezaji wa majukumu kwa mwaka wa fedha 2025/26 pamoja na mipango na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Nao watumishi wa GST walipata fursa ya kutoa maoni, ushauri na mapendekezo mbalimbali yaliyolenga kuboresha utoaji wa huduma, kuongeza ufanisi wa taasisi na kuendelea kuijengea GST uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.