Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mlezi wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) Mhe. Hamza S. Johari amesema kuwa Chama cha Mawakili wa Serikali kitaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuisaida Serikali kufikia malengo mbalimbali ambayo Serikali imejiwekea.

Mhe. Johari ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili wa Serikali wa Tanzania (TPBA), Jijini Arusha tarehe 13 Julai, 2026.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa Chama cha Mawakili wa Serikali nchini, kimeendelea kukua, kuimarika na kuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu wa kitaaluma, kujenga uwezo wa wanachama wake, kuimarisha maadili ya kazi, na kukuza ushirikiano miongoni mwa Wanasheria wa Serikali wanaotekeleza majukumu yao katika taasisi mbalimbali za umma.

“Chama Bora Cha Kitaaluma ni kile kinachosaidia Serikali katika kufikia malengo yake na sio kuitikisa au kuiyumbisha Serikali.”* Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Akieleza juu ya malengo ya Mkutano huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa Mkutano huo unalenga kutoa fursa kwa wanachama kujadili masuala mbalimbali yanayohusu chama hicho, maendeleo ya sekta ya sheria kwa ujumla pamoja na kufanya uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Mawakili wa Serikali.

Aidha, Mhe, Johari amesema kuwa pamoja na mafanikio mengine mengi yaliyofikiwa, Chama hicho kimeweza kuzindua Kitabu cha Falsafa ya Sheria ya Mama Samia ambacho kinaeleza kwa kina namna maboresho mbalimbali yaliyofanyika katika Sekta ya Sheria yalivyoleta mabadiliko katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Ameeleza kuwa, Kitabu hicho kinaelezea mwelekeo ulioonekana katika Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutumia sheria, sera, taasisi na mifumo ya utekelezaji kujenga mazingira ya maridhiano, uwekezaji, uwazi, huduma, haki, na maendeleo ya wananchi. 

*“Mwelekeo huu haukuonekana katika sekta moja tu. Umeonekana katika kodi na mapato, uwekezaji, nishati, ardhi, TEHAMA, utalii, elimu, msaada wa kisheria, hifadhi ya jamii, utawala bora, PPP na maeneo mengine mengi.”* Amesema Mhe. Johari

Katika hatua nyingine, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ina wajibu wa kuishauri Serikali kuhusu masuala ya sheria, mikataba, utungaji wa sheria, tafsiri ya sheria, na kulinda maslahi ya umma.

*“Ushauri wa sheria una thamani zaidi pale unaposaidia Serikali kufanya maamuzi yanayolinda maslahi ya taifa, yanayoleta maendeleo, yanayopunguza migogoro, yanayovutia uwekezaji na yanayowezesha wananchi kupata haki kwa wakati na kupata huduma bora.”*

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amesema kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 unahitaji uwepo wa sheria bora zinazoshabihiana na Dira na nguvu za kiuchumi, ambapo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaendelea kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kushabihisha sheria mbalimbali na Dira 2050.

Mhe. Johari ameeleza kuwa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea kuratibu na kushirikiana na wadau wote katika kuboresha sheria, kusimamia upatikanaji wa haki kwa wakati, kuimarisha ushauri wa kisheria kwa Serikali, kusimamia mikataba, na kuhakikisha kuwa sheria zinaendelea kuwa chombo cha maendeleo ili hatimaye malengo ya Dira 2050 yaweze kufikiwa.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali amemshukuru, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoendelea kuboresha mazingira ya utendaji kazi katika Sekta ya Sheria hususan Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

*“Mhe. Rais tunaendelea kukushukuru kwa namna ambavyo unaendelea kuboresha mazingira ya utendaji kazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kweli tunakushukuru sana sasa hivi mazingira yetu yameboreshwa sana.*

Amesema Mhe. Johari Mkutano Mkuu wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) uliofunguliwa leo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan unafanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 13 hadi 14 Julai, 2026 na umebeba kauli mbiu isemayo “Haki, Wajibu na Utawala wa Sheria ni Msingi wa Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050”.