Bodi ya Wakurugenzi Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro ikiongozwa na makamu Mwenyekiti Dkt. Harriet Mtae jana tarehe 11 julai, 2026 imekagua uboreshaji wa miundombinu ya utalii eneo la Nyayo za Laetoli lililopo hifadhi ya Ngorongoro 

Wakiwa Laetoli Wakurugenzi hao wamekagua uhifadhi wa Nyayo zilizogundulika katika eneo hilo miaka zaidi ya milioni 3.6 iliyopita na kuangalia hatua za utekelezaji wa mradi wa Geopark unaohusisha ujenzi wa jengo la kupokelea wageni, jengo la kupumzika wageni, jengo lililojengwa kwa ajili ya kuhifadhi Nyayo sambamba na miundombinu mingine.

Naibu Kamishna wa Uhifadhi Joas Makwati anayesimamia uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii ameeleza kuwa ziara hiyo imelenga kutathmini utekelezaji wa miradi inayofanywa na mamlaka kwa lengo la kuimarisha shughuli za uhifadhi, kuboresha huduma za utalii na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Hifadhi ya Ngorongoro.

Pamoja na kukagua miundombinu ya utalii wakurugenzi hao wamepokea taarifa ya hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na mipango ya kuendelea kuboresha mazingira ya utalii na shughuli za uhifadhi.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA, Dkt. Harieth Mtae, alisema miradi hiyo inaakisi dhamira ya mamlaka ya kuendelea kuwekeza katika uboreshaji wa vivutio vya utalii na kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wageni.

Ameongeza kuwa maboresho hayo yanatarajiwa kuongeza thamani ya vivutio vya utalii, kuvutia watalii zaidi na kuendelea kuitangaza Hifadhi ya Ngorongoro kama moja ya vivutio vinavyoongoza duniani.