Na Mwandishi Wetu

Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice M.S. Mafumiko, ametembelea banda la Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Julai 6, 2026, yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, ambapo amejionea huduma na shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na mamlaka hiyo katika kulinda afya ya wananchi.

Akiwasili katika banda hilo, Dkt. Mafumiko alipokelewa na Meneja wa Kitengo cha Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa TMDA, Gaudensia Simwanza, ambaye alimkaribisha na kumpa maelezo kuhusu shughuli zinazotekelezwa na mamlaka hiyo, ikiwemo usimamizi wa ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba, vitendanishi pamoja na bidhaa nyingine za afya. Pia alielezwa kuhusu elimu inayotolewa kwa wananchi kupitia Maonesho ya Sabasaba ili kuongeza uelewa wa matumizi sahihi ya dawa na umuhimu wa kutumia bidhaa za afya zilizosajiliwa.

Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Dkt. Mafumiko ameipongeza TMDA kwa kazi kubwa inayoifanya ya kuhakikisha dawa, vifaa tiba na bidhaa nyingine za afya zinazowafikia wananchi zinakuwa salama, zenye ubora na ufanisi. Amesema mamlaka hiyo imeendelea kutekeleza wajibu wake kwa weledi huku ikitoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya bidhaa za afya, jambo linalochangia kulinda afya za Watanzania. Aidha, amesisitiza TMDA kuendelea kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali na kutumia majukwaa kama Maonesho ya Sabasaba kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa elimu ya udhibiti wa bidhaa za afya.

Katika ziara hiyo, Dkt. Mafumiko amekabidhiwa kitabu maalumu cha maadhimisho ya miaka 20 ya TMDA, kinachoelezea safari ya mamlaka hiyo tangu ilipoanzishwa, mafanikio iliyoyapata katika kuimarisha udhibiti wa dawa, vifaa tiba na bidhaa nyingine za afya, pamoja na mchango wake katika kulinda afya ya Watanzania.