Na Mwandishi Wetu, Arusha
Wadau wa sekta ya kilimo, biashara, mazingira na teknolojia kutoka ndani na nje ya Afrika wanatarajiwa kukutana jijini Arusha katika Mkutano wa Kwanza wa Uchavushaji Afrika, unaolenga kuweka mkakati wa pamoja wa kulinda wachavushaji na kuimarisha kilimo endelevu barani Afrika.
Mkutano huo unatarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 29 hadi Oktoba 1, 2026, ukiandaliwa na Shirika la Maendeleo Endelevu ya Kilimo na Biashara za Kilimo Tanzania (SAADIT) kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali, ikiwemo Green Rural Community and workers bees Africa huku ukipata utambuzi rasmi kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara.
Kupitia mkutano huo, wadau watajadili changamoto na fursa zinazohusu uchavushaji, pamoja na namna ya kuingiza uhifadhi wa wachavushaji katika sera na mipango ya maendeleo ili kuongeza uzalishaji wa mazao, kuimarisha usalama wa chakula na kukuza uchumi wa kilimo.
Mkurugenzi na Mwanzilishi wa SAADIT, Malulu Martin Igobeko, amesema kupungua kwa idadi ya wachavushaji kutokana na uharibifu wa mazingira na matumizi yasiyo sahihi ya viuatilifu ni tishio kwa mifumo ya uzalishaji wa chakula barani Afrika.
Amesema mkutano huo utakuwa jukwaa la kuunganisha serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo katika kutafuta suluhisho la changamoto hiyo na kuhakikisha huduma za uchavushaji zinalindwa kwa maendeleo ya kilimo.
“Wachavushaji wanapungua kwa kasi kutokana na uharibifu wa maeneo wanayoishi na matumizi yasiyo sahihi ya viuatilifu. Bila wao, uzalishaji wa mazao na usalama wa chakula unaweza kuathirika,” amesema Igobeko.
Kwa upande wake, Genya Charles kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, amesema uchavushaji unapaswa kuonekana kama sehemu muhimu ya uchumi wa kijani na biashara, kutokana na mchango wake katika kuongeza thamani ya mazao na kufungua fursa za uwekezaji.
Naye Mercy Butta kutoka Idara ya Usalama wa Chakula katika Wizara ya Kilimo, amesema mchango wa nyuki na wachavushaji wengine ni muhimu katika kuongeza uzalishaji wa mazao na kuimarisha upatikanaji wa chakula nchini.
Katika mkutano huo, kampuni ya teknolojia ya ufugaji nyuki kutoka Australia, BeeSTAR Technology, inatarajiwa kuonyesha teknolojia za kisasa ikiwemo mizinga janja, matumizi ya akili bandia na mifumo ya kidijitali ya kufuatilia uzalishaji wa nyuki.
Teknolojia hizo zinatarajiwa kusaidia kuongeza uzalishaji wa asali, kupunguza upotevu wa mizinga na kuboresha huduma za uchavushaji katika sekta ya kilimo.
Aidha, mkutano huo utaangazia mpango wa kuongeza mizinga milioni moja unaolenga kuimarisha huduma za uchavushaji katika maeneo ya kilimo kupitia ushirikiano wa wadau mbalimbali.
Washiriki wa mkutano huo wakiwemo Green Rural Community and workers bees Africa wanatarajiwa kujadili masuala ya utafiti, teknolojia, sera, uwekezaji na mikakati ya maendeleo kwa kushirikisha taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa.

