
Mhadhiri Msaidizi wa Shule ya Uuguzi, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Hamza Lilenga, akionesha namna ya kutatua tatizo la kupumua kwa watoto wachanga baada ya kuzaliwa katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayofanyika kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, 2026.
Mbunifu kutoka MUHAS, Swahifat Ibrahim akionesha bidhaa ya Biosafe, ambayo ni kiuatilifu hai kinachosaidia kudhibiti wadudu na magonjwa ya mazao ya chakula.


Mwanafunzi wa MUHAS, Tulinave Aroha, akitoa ufafanuzi wa matumizi ya kifaa Tiba kiitwacho SIKU SMART, kinacholenga kuwasaidia wanawake kufuatilia mzunguko wa hedhi kwa usahihi.
………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimebuni teknolojia mbalimbali za kisasa zinazolenga kulisaidia taifa kutatua changamoto za kiafya na kilimo. Miongoni mwa ubunifu huo ni vifaa vya kisasa vinavyosaidia watoto wachanga kupumua baada ya kuzaliwa, mfumo wa kuwasaidia wanawake kufuatilia mzunguko wa hedhi, pamoja na teknolojia zinazoboresha matibabu ya saratani ya matiti.
Akizungumza Julai 4, 2026, katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, 2026, Mhadhiri Msaidizi wa Shule ya Uuguzi MUHAS, Hamza Lilenga, amesema kuwa chuo hicho katika maonesho hayo kinaonesha vifaa vya kisasa pamoja na bunifu mbalimbali.
Amesema kuwa wamekuja na vifaa tiba inavyosaidia watoto wachanga wanaopata changamoto ya kupumua mara baada ya kuzaliwa, pamoja na vifaa vinavyosaidia katika matibabu ya watoto wanaopata ugonjwa wa manjano.
Lilenga amesema kuwa kutokana na ongezeko la visa vya saratani ya matiti nchini, MUHAS imeendelea kuwajengea uwezo wanafunzi wake kutumia teknolojia na vifaa vya kisasa vya kitabibu ili kuboresha huduma na kurahisisha matibabu ya ugonjwa huo.
“Natoa wito kwa jamii kuwa na utamaduni wa kupima afya mara kwa mara ili kuhakikisha wanaishi maisha yenye afya njema,” amesema Lilenga.
Kwa upande wake, mbunifu kutoka MUHAS, Swahifat Ibrahim, amesema kuwa katika maonesho hayo amewasilisha ubunifu unaoitwa Biosafe, ambao ni kiuatilifu hai kinachosaidia kudhibiti wadudu na magonjwa ya mazao ya chakula.
Ibrahim amesema kuwa Biosafe ni kiuatilifu cha asili kinachotokana na vimelea hai, kinachosaidia kupunguza matumizi ya viuatilifu vya kemikali pamoja na athari zake kwa mazingira kupitia mkabala wa Afya Moja (One Health), unaozingatia afya ya binadamu, wanyama na mazingira kwa pamoja.
“Biosafe inafaa kutumika katika kilimo hai (organic farming) na kilimo cha kawaida (conventional farming),” amesema.
Amefafanua kuwa matumizi ya Biosafe yatasaidia kupunguza upotevu wa mazao ya chakula unaosababishwa na magonjwa ya mimea, hivyo kuchangia kuongeza usalama wa chakula na kukabiliana na changamoto ya upungufu wa chakula duniani.
Naye mwanafunzi wa MUHAS, Tulinave Aroha, amesema kuwa chuo hicho pia kimebuni kifaa kiitwacho SIKU SMART, kinacholenga kuwasaidia wanawake kufuatilia mzunguko wa hedhi kwa usahihi.
Ameeleza kuwa teknolojia hiyo itawasaidia wanawake wanaotamani kupata ujauzito pamoja na wale wanaotaka kuepuka mimba zisizotarajiwa.
Ameongeza kuwa ubunifu huo utawanufaisha wanafunzi wa kike na wanawake wanaoishi maeneo ya vijijini, ambako upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu afya ya uzazi bado ni changamoto.
Amesema kuwa kupitia programu za elimu shuleni walibaini wasichana wengi hawakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu namna ya kufuatilia mzunguko wao wa hedhi, jambo lililowachochea kufanya utafiti na kubuni kifaa cha SIKU SMART.
Kwa sasa, kifaa hicho kipo katika hatua za mwisho za usajili, huku wadau mbalimbali wakihimizwa kuwekeza zaidi ili kuongeza uzalishaji na kuhakikisha kinawafikia wanawake wengi nchini.
