Dar es Salaam – Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, amesema hakuna Bunge ambalo linaweza kuitwa dhaifu au lisilo na meno, akisisitiza kuwa Bunge lolote hutekeleza majukumu yake ya msingi ya kuisimamia Serikali, kutunga sheria na kuwakilisha wananchi kwa mujibu wa Katiba na kanuni.

Akizungumza na wahariri kuelekea maadhimisho ya miaka 100 ya historia ya Bunge, Zungu alisema mjadala unaodai Bunge la sasa ni dhaifu hauna msingi, kwani majukumu yake yameendelea kutekelezwa kama ilivyokuwa kwa mabunge yaliyopita.

Alisema katika kipindi chote cha uongozi wake, amekuwa akitoa nafasi sawa kwa wabunge wa upinzani kushiriki mijadala na shughuli za Bunge licha ya idadi yao kuwa ndogo, akisisitiza kuwa demokrasia imeendelea kuzingatiwa.

“Ndugu zangu kuna mambo yanaendelea na kuibuliwa na baadhi ya vyama vya upinzani. Kumbukeni mwaka 2015 Katiba ilikuwa ileile ambapo wabunge wa upinzani walikuwa 102 ambapo kati ya hao Chadema walikuwa 69.

“Tena wakati wanashinda Tume ya Uchaguzi kwa wakati ule haikuwa na maboresho na kambi rasmi ya upinzani ikatambulika.

“… kwanini Bunge lile lilikuwa na nguvu, lakini nini maana yake mjadala hapa chama kimoja (hakutaja jina) chama kimoja kilipata mgombea toka CCM katika uchaguzi wa mwaka 2015 jambo lililowasaidia kuimarika zaidi na kupata wabunge wengi. Sasa wapo wapinzani lakini hawajaimarika,” alisema.

Aliongeza kuwa hata katika ngazi za serikali za mitaa, vyama vya upinzani viliwahi kushinda na kuongoza halmashauri mbalimbali za Dar es Salaam zikiwemo Kinondoni, Ubungo na Ilala, jambo lililoonyesha kuwa mazingira ya kisiasa yaliwaruhusu kushindana na kushinda.

Akijenga hoja yake, Zungu alisema kazi kuu ya Bunge imeendelea kuwa ni kuisimamia Serikali, kulinda ustawi wa wananchi na kutunga sheria, hivyo hakuna sababu ya kuligawa Bunge katika makundi ya “dhaifu” au “imara” kwa kuwa wajibu wake umebaki uleule.

Spika huyo alieleza kuwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, vyama vya upinzani vina jumla ya wabunge tisa pekee, hali inayofanya kushindwa kutimiza matakwa ya kanuni yanayohitaji wabunge 10 ili kuunga mkono hoja inayowasilishwa.

“Zipo hoja nzuri huyu hapa Ado (Mbunge wa Tunduru ACT) hata akitoa hoja wanakuwa tisa wakati kanuni inataka wawe 10,” alisema.

Hata hivyo, alisema pamoja na uchache huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alielekeza Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuendelea kuongozwa na wabunge wa upinzani kama sehemu ya kuimarisha demokrasia nchini.

“Ni nani asiyejua kwamba Rais Dkt. Samia ndiye amewarudisha nchini wapinzani wengine waliokimbia nchi kwa kuwataka warudi ili tujenge Taifa letu, haya ni mapenzi makubwa ya Rais Samia.

“Hata mnaposikia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali lakini kamati ambayo kwenye mpira tunaita kamati ya saa 72, kwa maana PAC na LAAC, ndio wajibu wa kumwita kila aliyetajwa,” alisema.

Kuhusu maadhimisho ya miaka 100 ya Bunge, Zungu alisema maandalizi yanaendelea, huku akieleza kuwa historia ya chombo hicho tangu kipindi cha ukoloni ni sehemu muhimu ya safari ya maendeleo ya demokrasia nchini.

“Wapo wengine watahoji kwa nini tunawataja wakoloni, lazima tuwataje ili tuone tulipotoka, tulipo na tunapokwenda.

“Kauli mbiu yetu katika kutimiza miaka 100 ya Bunge ni ‘Historia Yetu, Dira Yetu,’” alisema.