Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Pili Mnyema wakati wa halfa ya kilele cha maadhimisho ya miaka 30 ya TRA ambapo katika ngazi ya Mkoa yalifanyika katika ukumbi wa shule ya uongozi Mwalimu Juliasi Nyerere Wilaya ya Kibaha na kuwakutanisha walipa kodi mbali mbali pamoja na wadau wa maendeleo, wananchi na viongozi wa viongozi wa dini.
Katika kilele cha maadhimisho hayo ambayo yalikuwa ya aina yake yalikwenda sambamba na kufuatilia matangazo yaliyokuwa yanarushwa moja kwa moja kufuatilia halfa ya utoaji wa tuzo za walipa kodi bora mbali mbali Tanzania ambazo zilikuwa zinatolewa na mgeni rasmi Rais Dkt. Samia Suluhu Hasssan Jijini Dar es Salaam.
“Nawapongeza sana TRA Mkoa wa Pwani kwa kuweza kutimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake maana haikuwa safari nyepesi mmeweza kuvuka milima na mabonde kwa hali na mali kwa hiyo kwa upande wangu nawapongeza sana na mzidi kuendelea kukusanya mapato kwa ajili ya kuweza kuisaidia serikali kupata mapato yake kihalali ambayo yatakwenda katika kusaidia katika kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo.”amebainisha Katibu Tawala.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Pwani Salim Makame amesema kwamba lengo lao kubwa ni kuzidi kuendelea kushirikiana bega kwa bega na walipa kodi wote na kuwawekea mazingira mazuri ambayo yataweza kuwasaidia katika kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
“Tumetimiza miaka 30 ya TRA tangu kuanzishwa kwake kwa hiyo kitu kikubwa sisi tutaendelea kushirikiana bega kwa bega na wadau pamoja na walipa kodi na kwamba kitu kikubwa zaidi tunaomba ushirikiano wenu ambao utaweza kutusaidia kwa upande wetu katika suala zima la ukusanyaji wa mapato kwa maendeleo ya Taifa letu hasa katika kipindi hiki tunapoanza mwaka mpya wa fedha ,”amebainisha Makame.

