Na Saidi Saidi, WMJJWM – Dar Es Salaam
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima, leo Juni 29, 2026, amemtembelea Victoria Mkwizu, mama aliyejifungua watoto watano kwa wakati mmoja katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, kwa lengo la kumjulia hali, kumpongeza na kumkabidhi zawadi mbalimbali. Zawadi hizo ni ishara ya upendo na faraja kwa familia hiyo katika kipindi hiki cha malezi ya watoto hao.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Gwajima amesema amefurahishwa na taarifa za mama huyo kujifungua salama pamoja na watoto wake watano, huku akimtakia afya njema mama huyo na watoto wake.
Aidha, Dkt. Gwajima ameipongeza Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa weledi, umahiri na huduma bora zilizowezesha mama huyo kujifungua salama pamoja na watoto wote watano kwani mafanikio hayo yanaakisi uwezo mkubwa wa wataalamu wa afya nchini pamoja na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kuendelea kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Gwajima amewaagiza Maafisa Ustawi wa Jamii kuendelea kuifuatilia familia hiyo kwa karibu, kutoa ushauri nasaha na kuhakikisha inapatiwa huduma stahiki za ustawi wa jamii, pamoja na kuunganishwa na fursa mbalimbali za kijamii zitakazowasaidia katika malezi na makuzi ya watoto hao.
Kwa upande wake, Victoria Mkwizu na mumewe wameishukuru Serikali pamoja na wadau mbalimbali waliojitokeza kuwapa pongezi, faraja na michango mbalimbali huku akimshukuru Waziri Dkt. Gwajima kwa kutenga muda wa kuwajulia hali kwani ziara hiyo imewapa faraja, matumaini na moyo wa kuendelea kuwalea watoto wao katika mazingira ya upendo, malezi bora na ustawi wa familia.

