Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Dkt. Jim Yonazi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa inayosimamia na kuratibu utekelezaji wa masuala mtambuka katika kupambana na afua za UKIMWI, Kifua Kikuu (TB), Malaria pamoja na Uimarishaji wa Mifumo endelevu ya Afya (RSSH), inayotekelezwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Dunia (Global Fund) nchini Tanzania ijulikanayo kama Tanzania National Coordination Mechanism – (TNCM), ameongoza kutano wa Kawaida wa Combo hicho wa robo ya pili ya mwaka 2026.
Mkutano huo umefanyika tarehe 29 Juni, 2026 katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Jijini Dar es Salaam ulihusisha wawakilishi wa wadau kutoka Serikalini, Mashirika yasiyo ya kiserikali, Asasi za Kiraia, na Washirika wa Maendeleo, kwa lengo la kupokea na kujadili taarifa ya hali ya Utekelezaji wa Miradi ya hiyo kwa Mzunguko wa saba (Januari 2024 hadi Disemba 2026) hadi kufikia Mei 30, 2026 pamoja na kujadili hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya maombi ya ufadhili wa Mfuko wa Dunia kwa Mzunguko wa Nane (GC8) unaotarajiwa kuanza Januari 2027 – hadi Disemba 2029.
Kupitia ufadhili wa Mfuko wa Dunia, Nchi imeweza kupiga hatua katika kuendelea kuimarisha afya za Watanzania hususani katika kutoa tiba pamoja na kinga dhidi ya magonjwa hayo pamoja na kuweka misingi imara ya upatikanaji wa rasilimali katika sekta ya afya nchini.
Dkt. Jim Yonazi, ameeleza kufurahishwa na namna ambavyo masuala haya yanaendelea kuratibiwa, amewashukuru wadau wote kushirikiana katika kusimamia na kuhakikisha Nchi inakuwa na Amani na kuwa na Taifa lenye afya bora.

