Katibu mkuu wa jumuiya ya Afrika Mashariki Balozi Stephen  Mbundi akizungumza kwenye mdahalo huo jijini Arusha.
……………
Na Happy Lazaro, Arusha.
Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamewataka wanawake vijana kutumia kikamilifu jukwaa la Mdahalo wa Kizazi kwa Kizazi wa Wanawake wa Afrika Mashariki kujieleza, kushiriki maamuzi na kusukuma ajenda ya usawa wa kijinsia pamoja na maendeleo ya kidijitali katika ukanda huo.
Akizungumza katika mdahalo huo, Katibu mkuu wa jumuiya ya Afrika Mashariki Balozi Stephen  Mbundi amesema kuwa ,ana matumaini makubwa matatu katika siku mbili za mkutano huo, akianza kwa kusisitiza umuhimu wa mazungumzo ya kweli kati ya vizazi tofauti. 
Amesema ni muhimu kuhakikisha majadiliano hayo hayageuki kuwa nafasi ya viongozi wakubwa kuzungumza huku vijana wakisikiliza kimya, bali yawe jukwaa la pande zote kusikilizana, kubadilishana uzoefu na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu changamoto zinazowakabili wanawake katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Alieleza kuwa ni muhimu viongozi waandamizi, wabunge, wataalamu, wanafunzi na wanawake wengine walioshiriki mkutano huo, iwe ukumbini au kwa njia ya mtandao, kupewa nafasi sawa ya kuchangia mijadala hiyo. 
Balozi Mbundi amewahimiza wanawake vijana kujitokeza kwa ujasiri, kutumia majukwaa waliyopewa na kushiriki kikamilifu katika kuamua mwelekeo wa matokeo ya mdahalo huo.
Aidha  amesema ni lazima mazungumzo hayo yazalishe matokeo ya vitendo kupitia mpango kazi ulio wazi, mahsusi na unaotekelezeka.
Amesisitiza kuwa waraka wa matokeo ya mkutano huo unapaswa kuwa na malengo yanayopimika, muda maalum wa utekelezaji na kuendana na sera, mikakati au miswada iliyopo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kila ahadi itakayowekwa iweze kutekelezwa kwa ufanisi.
Ameongeza kuwa ahadi zenye mwelekeo wa utekelezaji ndizo zenye uwezo wa kuleta mabadiliko ya kweli katika maisha ya wanawake na wasichana wa Afrika Mashariki.
 Amefafanua kuwa , mkutano huo unapaswa kuwa mwanzo wa hatua mpya ya kuhakikisha kuwa maamuzi yanayofikiwa hayaishii kwenye makabrasha na hotuba, bali yanageuka kuwa sera na hatua halisi zinazogusa maisha ya wananchi.
Aidha  mdahalo huo umefanyika katika kipindi muhimu ambapo utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) unaelekea kwenye ukomo wake, hivyo kuna haja ya kuhakikisha viashiria vya usawa wa kijinsia vinabaki kuwa sehemu ya vipaumbele vya maendele.
 “Maamuzi yatakayofikiwa katika mkutano huo yanapaswa kuwafikia wanawake na wasichana walioko katika mazingira magumu, ambao mara nyingi sauti zao hazisikiki lakini ndio wanaohitaji zaidi matokeo ya mijadala hiyo.”amesema Balozi Mbundi.
Aidha ametoa shukrani kwa washirika mbalimbali waliofanikisha kufanyika kwa mdahalo huo na kusisitiza kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki itaendelea kushirikiana nao katika kuendeleza ajenda ya uwezeshaji wa wanawake.