Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma Joseph Kashushura aliyevaa kapelo,akimsikiliza katibu wa afya wa Halmashauri hiyo George Mhina kulia,baada ya kukagua ujenzi wa kituo cha afya Langiro kata ya Langiro.

Baadhi ya watumishi wa kituo cha afya Langiro kata ya Langiro, wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Hamashauri ya wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma Joseph Kashushura baada ya kukagua mra.

Muonekano wa baadhi ya majengo ya kituo kipya cha afya Langiro Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma kilichojengwa ili kusogeza na kuboresha huduma za matibabu kwa wananchi wa kata ya Langiro.

………

Na Mwandishi Wetu, Mbinga

WAKAZI wa kata ya Langiro na maeneo jirani katika halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma,wameanza kupata huduma bora za afya baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha afya Langiro.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Mbinga Joseph Kashushura amesema,katika mradi huo Serikali kuu imetoa Sh.milioni 632 na Halmashauri ya wilaya imeongeza Sh.milioni 50 kutoka mapato ya ndani ili kuhakikisha kituo hicho kinakamilika haraka.

Kwa mujibu wa Kashushura,mradi huo wa kituo cha afya umehusisha jengo la wagonjwa wa nje,matundu ya choo,kichomea taka wodi za kulaza wagonjwa ikiwemo wodi za mama wajawazito na watoto,maabara na jengo la kufulia.

Amesema,lengo ni kusogeza na kuboresha huduma za afya karibu na wananchi, kupunguza gharama,muda wa kusafiri kufuata matibabu,kuimarisha huduma kinga na tiba kwa wananchi na kupunguza msongamano katika vituo vingine vya afya vilivyopo.

Amesema, kukamilika kwa mradi huo ni ukombozi mkubwa kwa wakazi wa eneo hilo ambao awali walilazimika kusafiri umbali mrefu kwenye maeneo mengine kufuata huduma za afya hususani huduma za wagonjwa wa nje(OPD)pamoja na afya ya mama na mtoto.

Kashushura ameongeza kuwa,vifaa tiba vyote muhimu vimeshafika pamoja na watumishi ambao wameanza kutoa huduma kwa wakazi wa vijiji mbalimbali vya kata ya Langiro na kata nyingine za jirani.

Kashushura ameongeza kuwa,Serikali ya awamu ya sita kazi yake ni kutoa huduma bora kwa wananchi wake,kwa hiyo kituo hicho ni nia nzuri ya Serikali katika kuhakikisha inasogeza huduma mbalimbali ambapo kuwataka wananchi kwenda kupata huduma za matibabu.

“Serikali kupitia Halmashari ya wilaya Mbinga inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya afya ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora na kwa wakati,bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu”alisema Kashushura.

Katibu wa afya wa Halmashauri hiyo George Mhina,amempongeza Mkurugenzi mtendaji wa Joseph Kashushuru kwa uthubutu wake kwani tangu amefika katika Halmashauri hiyo uimarishwaji wa huduma za afya umekuwa mkubwa.

“Katika Halmashauri yetu vituo vya afya vilivyokuwa vinafanya kazi ni viwili,lakini sasa kuna vituo sita vya Serikali ambavyo vinatoa huduma za afya,Halmashauri imeweka mkazo zaidi katika kuhakikisha huduma ya mama na mtoto inaimarishwa na kwenye vituo vyote huduma ya upasuaji ikiwemo ya mama wajawazito inatolewa”alisema Mhina.

Amemshukuru Kashushura kwa kukamilisha miradi viporo ya zahanati zilizoanzishwa na wananchi kwani kati ya maboma 32 yaliyokuwepo awali,maboma 17 yamekamilika na mkakati wa Halmashauri ni kumaliza ujenzi wa maboma yaliyobaki.

Amewapongeza wananchi wa Halmashauri ya wilaya Mbinga,kwa ushirikiano mkubwa katika ujenzi wa miradi mbalimbali inayoanzishwa na kuwaomba kutembelea vituo vya afya na zahanati zilizojengwa kwa ajili ya kupata huduma za afya,ustawi wa jamii na lishe ili kuimarisha afya zao.

Mhina amesema, kukamilika kwa kituo cha afya Langiro kunatarajiwa kuongeza ubora wa huduma za afya,kuokoa maisha ya wananchi kwa kuwafikishia huduma kwa wakati na kuchochea maendeleo ya kijamii katika kata hiyo na maeneo jirani.

Kwa upande wake mganga mfawidhi wa kituo cha afya Langiro Domina Mazengo amesema,wameanza kutoa huduma ya magonjwa mbalimbali ya kuambukiza na yasiyoambukiza kama kisukari ambayo awali wananchi walilazimika kwenda maeneo mengine kufuata huduma.

Mkazi wa kijiji cha Kipapa Alois Masiha,ameishukuru Serikali kujenga kituo cha afya Langiro ambacho kimesaidia kupata huduma za matibabu karibu hasa ikizingatia kuwa awali walilazimika kwenye kata nyingine kama Mapera na Maguu ili kufuata huduma hizo.