Tanzania imeendelea kujijengea heshima katika jukwaa la kimataifa baada ya kutambuliwa kama mfano wa kuigwa katika kuimarisha haki za wanawake wakiwemo wafanyakazi wa majumbani, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake wa Kidiplomasia ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika Geneva, Uswis.
Utambuzi huo umetolewa katika Mjadala wa Haki za Binadamu kuhusu Haki za Wanawake uliofanyika pembeni mwa Kikao cha 62 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kinachoendelea mjini Geneva kuanzia tarehe 15 Juni hadi 7 Julai 2026.
Akizungumza kwa niaba ya Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Mkurugenzi wa Kitengo cha Jinsia, Usawa na Ushirikishwaji katika Shirika la Kazi Duniani (ILO), Bi. Chidi King, ameipongeza Tanzania kwa ushirikiano wake na ILO katika kutekeleza programu zinazowawezesha wafanyakazi wa majumbani kutambua, kulinda na kutetea haki zao.
Bi. King amesema juhudi hizo zimechangia kuwajengea wanawake uwezo wa uongozi, kujiamini na kushiriki kikamilifu katika maamuzi yanayogusa maisha yao, hatua ambayo imewezesha sauti zao kusikika zaidi katika jamii na maeneo ya kazi.
Amesema mafanikio hayo yanaonesha dhamira ya Serikali ya Tanzania katika kukuza usawa wa kijinsia na kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa za kushiriki katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Utambuzi huo unaakisi hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Tanzania za kuwawezesha wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi, shughuli za kidiplomasia na sekta nyingine muhimu za maendeleo, sambamba na kulinda haki zao za msingi.
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake wa Kidiplomasia ya Umoja wa Mataifa, yanayoadhimishwa tarehe 24 Juni kila mwaka, yamelenga kutambua mchango wa wanawake katika diplomasia na ujenzi wa dunia yenye usawa, amani na maendeleo endelevu.
Kwa upande wa Tanzania, mjadala huo ulihudhuriwa na Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Geneva, Bi. Hoyce Temu, ambaye alishiriki katika maadhimisho hayo yaliyokusanya viongozi, wanadiplomasia na wadau mbalimbali wa haki za binadamu kutoka mataifa tofauti duniani.
