Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam

Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la International Media Support (IMS), umeahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano na vyombo vya habari pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya habari nchini ili kukuza uandishi wa habari zenye maslahi kwa umma.

Akizungumza wakati wa semina iliyowakutanisha wawakilishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, Mkurugenzi wa UTPC, Kenneth Simbaya, alisema ushirikiano kati ya wadau wa sekta ya habari ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na zenye manufaa kwa maendeleo yao.

Alisema kuna haja ya kuimarisha ushirikiano kati ya vyombo vya habari, mamlaka za usimamizi wa sekta hiyo na wadau wengine ili kuleta mabadiliko chanya yatakayochochea upatikanaji wa habari zinazolenga maslahi ya wananchi.

“Tunao wajibu wa kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha tunajenga jamii yenye taarifa sahihi. Kila mmoja anatakiwa kutimiza wajibu wake ili kufikia malengo ya kuimarisha sekta ya habari nchini,” alisema Simbaya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tanzania Media Foundation Dastan Kamanzi (TMF), alisema waandishi wa habari wanapaswa kuweka kipaumbele katika kuandaa na kuchapisha habari zinazogusa maisha ya wananchi, haki zao pamoja na uhuru wao.

Alieleza kuwa kufanya hivyo kutasaidia kuitendea haki taaluma ya uandishi wa habari na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya jamii.

Wakichangia mjadala huo, baadhi ya wawakilishi wa vyombo vya habari walieleza kuwa utekelezaji wa habari za maslahi kwa umma unahitaji uwezeshaji zaidi kupitia mafunzo na upatikanaji wa vitendea kazi vya kisasa.

Walisema baadhi ya vyombo vya habari bado vinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa wataalamu wenye ujuzi wa kutumia mbinu za kisasa katika kuandaa na kuandika habari za maslahi kwa umma.

Semina hiyo iliyoandaliwa na UTPC ililenga kufanya tathmini ya pamoja kuhusu changamoto zinazoathiri upatikanaji wa habari za maslahi kwa umma na kujadili mikakati ya kuzitatua. Semina hiyo ilifanyika Juni 19, 2026 katika Hoteli ya Mbezi Garden, jijini Dar es Salaam.