Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog,Dodoma
Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu katika Wizara ya Viwanda na Biashara, Saidi Musa Msabimana, amesema kuwa wizara hiyo pamoja na taasisi zake nane zinazoiwakilisha katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma zinatoa huduma mbalimbali kwa wananchi na kuwahimiza kutembelea mabanda yao ili kupata elimu na huduma zinazotolewa.
Akizungumza Juni 17, 2026 katika Banda la Wizara ya Viwanda na Biashara kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, Amesema kuwa miongoni mwa taasisi zinazoshiriki maonesho hayo ni BRELA, ambayo inatoa huduma za usajili wa makampuni, majina ya biashara na alama za biashara, huku Wakala wa Stakabadhi za Maghala ukiendelea kutoa huduma za usajili na utoaji wa leseni za uendeshaji wa maghala.
Msabimana amebainisha kuwa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) pia kinashiriki maonesho hayo kwa lengo la kutoa taarifa kuhusu fursa za elimu ya biashara, huku akiwaalika wananchi kuwapeleka vijana wao chuoni hapo ili kupata elimu bora ya biashara.
Aidha, amesema kuwa Wakala wa Vipimo unaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuzingatia vipimo sahihi vya bidhaa mbalimbali ili kulinda maslahi ya walaji na kuhakikisha wanapata bidhaa zinazokidhi viwango vinavyotakiwa.
Pia ameongeza kuwa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) linatumia maonesho hayo kutoa taarifa kuhusu maendeleo ya miradi ya kimkakati inayosimamiwa na shirika hilo ikiwemo Liganga, Mchuchuma na Soda Ash.
Amesema kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara ni miongoni mwa wizara zinazoratibu miradi mikubwa ya kimkakati yenye mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Vilevile, ameeleza kuwa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) linaendelea kutoa elimu kuhusu mikopo ya vijana iliyotolewa na Serikali, huku wananchi hususan vijana wakihimizwa kutembelea banda la taasisi hiyo ili kujifunza taratibu za kupata na kutumia mikopo hiyo kwa manufaa yao.
Msabimana amesema kuwa Tume ya Ushindani (FCC) nayo inashiriki maonesho hayo kwa lengo la kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa ushindani wa haki katika biashara.
Aidha, amewataka wananchi kutembelea mabanda ya wizara na taasisi zake ili kupata elimu kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa pamoja na mipango ya maendeleo inayotekelezwa katika sekta za viwanda, biashara na maendeleo ya viwanda vidogo.
Kuhusu usajili wa biashara na bunifu, Msabimana amesema kuwa kutokusajili biashara au bunifu kunawaweka wahusika katika hatari ya kupoteza haki zao za umiliki pale watu wengine wanapoweza kunakili na kusajili bunifu hizo kwa majina yao.
Amesema kuwa BRELA inaendelea kutoa huduma za usajili katika maonesho hayo na kwamba wananchi wanaokidhi masharti wanaweza kupata huduma hizo ndani ya muda mfupi.
Akizungumzia Wakala wa Vipimo, Msabimana amebainisha kuwa taasisi hiyo inalenga kumlinda mlaji kwa kuhakikisha bidhaa zinazouzwa zinazingatia vipimo sahihi.
Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kupata elimu ya vipimo ili waweze kutambua bidhaa zisizokidhi viwango, akitolea mfano mitungi ya gesi na nondo ambazo wakati mwingine zinaweza kutofautiana na viwango vinavyoelekezwa.
Aidha, amesema kuwa matumizi ya bidhaa zisizokidhi vipimo yanaweza kusababisha hasara kwa walaji na kuhatarisha usalama, hususan katika sekta ya ujenzi ambapo matumizi ya nondo zisizo na viwango vinaweza kuongeza hatari katika majengo.

