Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog,Dodoma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua Awamu ya Pili ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia itakayofanyika Juni 20, 2026 katika Viwanja vya Dole, Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari Juni 17, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera, amesema kuwa kampeni hiyo ni utekelezaji wa maono na maelekezo ya Rais Samia ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma za msaada wa kisheria na haki zao kwa wakati.
Amesema kuwa kampeni hiyo ilianzishwa baada ya Rais Samia kubaini kuwa wananchi wengi wanakosa haki zao kutokana na kutofahamu sheria na kushindwa kupata msaada wa kisheria wanapokumbana na changamoto mbalimbali za kisheria.
Dkt. Homera amebainisha kuwa katika awamu ya kwanza ya kampeni hiyo, zaidi ya wananchi milioni nne walifikiwa nchini kote, huku Zanzibar pekee wananchi 422,908 wakinufaika na huduma za msaada wa kisheria, wakiwemo wanawake 209,185 na wanaume 213,723.
Aidha, amesema kuwa awamu ya pili inalenga kuwafikia wananchi wengi zaidi kupitia utoaji wa huduma katika mikoa yote 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar, wilaya zote, kata zote, vijiji na vitongoji.
Ameongeza kuwa uzinduzi wa kampeni hiyo Zanzibar una lengo la kuendelea kuimarisha Muungano kwa kuhakikisha huduma za msaada wa kisheria zinawafikia Watanzania wote bila ubaguzi.
Dkt. Homera amesema kuwa maandalizi ya uzinduzi huo yamekamilika kwa asilimia 100 na kwamba zaidi ya wananchi 15,000 hadi 20,000 wanatarajiwa kushiriki katika hafla hiyo.
Amebainisha kuwa kampeni hiyo itatoa msaada wa kisheria katika masuala mbalimbali ikiwemo ndoa, talaka, mirathi, unyanyasaji wa kijinsia, haki za wafanyakazi pamoja na migogoro mingine ya kisheria na kijamii.
Aidha, amesema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha haki zilizopotea kwa wananchi zinarejeshwa bila kujali dini, kabila, itikadi za kisiasa au maeneo wanayotoka.
Kaulimbiu ya kampeni hiyo ni “Msaada wa Kisheria kwa Haki, Amani na Maendeleo.”
“Tunaamini popote penye haki na usawa kuna maendeleo. Sheria ni maisha yako; kila hatua unayopitia inaongozwa na sheria. Hivyo kila Mtanzania anapaswa kufahamu haki zake na kutimiza wajibu wake,” amesema Dkt. Homera
Ameongeza kuwa kupitia kampeni hiyo, wananchi watapata elimu ya sheria, ushauri wa kisheria na huduma mbalimbali zitakazowasaidia kutatua changamoto zinazowakabili na kupata haki zao kwa mujibu wa sheria za nchi.

