Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amesema Serikali imeendelea kuboresha ustawi wa watumishi wa umma ambapo kwa mwaka 2025/26 jumla ya watumishi 219,000 waliopandishwa vyeo baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa.Akizungumza Juni 17, 2026 Jijini Dodoma, wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Mhe. Kikwete amesema Serikali itaendelea kuhakikisha watumishi wanatambuliwa kutokana na sifa na utendaji wao ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Aidha, amesema zoezi la upandishaji vyeo linapaswa kuendelea kutekelezwa kwa kuzingatia Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma, sheria na miongozo husika ili kuondoa upendeleo na uonevu kwa watumishi.

Amebainisha kuwa pamoja na mafanikio hayo, bado zipo changamoto zinazokwamisha baadhi ya watumishi kupata stahiki zao kwa wakati, ikiwemo baadhi ya waajiri kuchelewa kuwasilisha majina ya watumishi wanaostahili kupanda madaraja katika Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Pia ameongeza kuwa baadhi ya taasisi zimekuwa hazifanyii watumishi tathmini za utendaji kazi kwa wakati kupitia mfumo wa e-Utendaji, hali inayowakosesha baadhi yao sifa za kupandishwa madaraja.

Kutokana na hali hiyo, Mhe. Kikwete amewaelekeza waajiri wote kuhakikisha watumishi wenye sifa ambao hawakufanyiwa tathmini lakini wanastahili kupanda madaraja, taarifa zao zinawasilishwa Ofisi ya Rais – Utumishi ili waweze kunufaika na haki hiyo.

Aidha, amesema Ofisi yake itachukua hatua stahiki dhidi ya wasimamizi watakaobainika kushindwa kuwafanyia tathmini watumishi wanaowasimamia kwa kuwa hatua hiyo ni sehemu ya uwajibikaji katika utumishi wa umma.

Amesema Serikali itaendelea kusimamia utendaji kazi na uwajibikaji kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma (e-Utendaji) ambao kwa sasa umeunganishwa na taratibu za kupandishwa vyeo na kuthibitishwa kazini.

Mhe. Kikwete amewataka watumishi wa umma kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa uwazi, uaminifu, weledi na ufanisi ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha utumishi wa umma nchini.