Na Mwandishi wetu, Mwanza
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza imetoa hukumu katika shauri la jinai Na. ECC 13121/2026 linalowakabili viongozi wa Chama cha Ushirika cha SUGECO cha Mkoa wa Morogoro, kwa makosa ya uhujumu uchumi yaliyosababisha hasara kwa serikali.
Katika hukumu iliyotolewa Juni 12, 2026, mahakama iliwatia hatiani Bw. Revocatus Vallery Kimario na Bw. Joseph Cyprian Masimba na kuamuru warejeshe kiasi cha Sh.106,000,000 kwenye akaunti ya TAKUKURU Wilaya ya Ukerewe, fedha ambazo walizisababishia serikali kupotea.
Mbali na kurejesha fedha hizo, mahakama pia iliwatoza faini ya Sh.100,000 kila mmoja kwa makosa hayo yaliyokiuka Kifungu cha 57(1) pamoja na vifungu vya 62(1) na 62(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200 Marejeo ya mwaka 2022.
Kesi hiyo iliendeshwa na waendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ambao ni Bw. Moses Malewo, Bw. Cosmas Magesa na Bi. Nyamaindi Lisso.
Shauri hilo lilisikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Mwanza, Mheshimiwa Marley.
