Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) yaagizwa kuharakisha zoezi la utiaji saini makubaliano baina yake na kampuni ya Superdoll Trailer Manufacture ili kuongeza umahiri wa wanafunzi na wahitimu wa mafunzo ya ufundi stadi kupitia kuwajengea uwezo wa mazingira halisi ya kazi na kuongeza ushindani wao katika soko la ajira nchini na nje ya nchi.
Wito huo umetolewa tarehe 6 Juni, 2026 na Mhe. Wanu Hafidh Ameir, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia katika ziara yake ya kutembelea na kujionea namna shughuli mbalimbali za uzalishaji zinavyofanyika kiwandani hapo pamoja na juhudi zinazofanyika katika kukuza ujuzi kwa wafanyakazi kupitia kitengo chao cha mafunzo ya ufundi stadi.
Akisoma hotuba fupi kwa uongozi wa kiwanda cha Superdoll na VETA katika ukumbi wa mikutano wa kiwanda hicho uliopo makao makuu, Tazara jijini Dar es salaam Mh. Wanu amesema amefurahishwa na namna ambavyo Superdoll imeweza kuunganisha shughuli za uzalishaji wa viwandani na maendeleo ya rasilimaliwatu kupitia mafunzo kwa vitendo wanayotoa ya kuendelea kuwajengea wafanyakazi na vijana uwezo na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na maendeleo ya sekta ya viwanda nchini.
“Serikali inaweka nguvu kubwa katika kuhakikisha vijana wanapata ujuzi unaotakiwa katika soko la ajira na Superdoll ni mfano bora wa ushiriki wa sekta binafsi katika kukuza ujuzi na kuanda nguvu kazi yenye tija, jambo ambalo serikali inalipa kipaumbele kikubwa katika juhudi zake za kujenga uchumi shidani na endelevu” amesema Mhe. Wanu.
Aidha, Mhe. Wanu amesema serikali ya awamu ya sita imeendelea kuhimiza ushirikiano wa karibu kati ya Taasisi za Elimu na sekta ya uzalishaji baada ya kuzindua mpango wa ushirikiano kati ya vyuo na viwanda kama hatua ya kujenga taifa lenye vijana wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira, hatua inayoakisi dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuimarisha ubora wa rasilimaliwatu kwa kuzingatia mabadiliko ya kiuchumi na kiteknolojia yanayoendelea duniani.
“Napenda kutumia fursa hii kuhimiza uimarishaji wa ushirikiano kati ya Superdoll na VETA ili wanafunzi na wakufunzi wa mafunzo ya ufundi stadi wapate fursa niyngi zaidi za mafunzo kwa vitendo kazini (industrial attachment), uongeze umahiri, kuwajengea uzoefu wa mazingira halisi ya kazi na kuimarisha ubora wa mafunzo yanayotolewa na kuongeza ushindani wao katika soko la ajira.
Akipokea wito kutoka kwa Mhe. Wanu, Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA. Anthony Kasore amesema VETA imekuwa ikishirikiana kwa karibu zaidi na Superdoll katika kuwapatia wanafunzi ujuzi na kuwajengea wakufunzi uwezo unaowasaidia pindi wanapokuwa wameajiriwa katika sekta za viwanda na maeneo mbalimbali.
“Sisi kama VETA tunawashukuru wenzetu wa Superdoll kwa ushirikiano tuliokuwa nao kwa zaidi ya miaka 30. Na asilimia 80% ya wanafunzi na wahitimu wetu wamekuwa wakiajiriwa hapa na wengine kupata maeneo ya kufanya mazoezi ya vitendo na hivyo kukubalika zaidi katika soko la ajira mara wanapohitimu mafunzo yao” aliongeza CPA.Kasore.
Aidha CPA.Kasore ameahidi ushirikiano huo katika utengenezaji wa mitaala itakayotoa mafunzo ya kuwajengea utaalamu zaidi wanafunzi na wakufunzi, kufundisha wanafunzi hatua stahiki za matumizi sahihi ya teknolijia za kisasa duniani ili kuendana na mkakati wa serikali wa mwaka 2026 unaohimiza ushirikiano kati ya taasisi za juu, vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi na viwanda nchini ili kuhakikisha wanazalisha wahitimu wenye weledi na maarifa ya stadi stahiki zinazohitajika katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.
Nae, Meneja Mkuu wa Superdoll ndugu, Ibrahim Juma Ally amsema kampuni hilo limekuwa na maono makubwa ya uwekezaji katika rasilimaliwatu kwa kuwajenga uwezo wa kitaalamu kupitia mafunzo yanayoendelea kwa takriban miongo mitatu(3) na kupitia ushirikiano na wadau mbalimbali ili waweze kuzalisha na kushindana katika soko laTanzania na nje.
“Sisi kama Superdoll tumewekeza katika vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia,tuna wakufunzi mahiri wenye mafunzo na maarifa kwenye teknolojia za kisasa na kimataifas katika kuandaa rasilimaliwatu. Lakini pia tunazungumzia ushirikiano na wadau mbalimbali wa serikali na wateja wetu ambao wote hao wanahitaji mafunzo ili kuweza kuendana na teknolojia mbalimbali zilizopo katika sekta ya usafirishaji, hivyo ushirikiano wetu na VETA unaweza kutupa morali zaidi ya kusonga mbele katika eneo hili” amesema ndugu, Ally.
Pamoja na wito huo kwa VETA, Mhe. Wanu pia ameelekeza Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) kufanya tathmini na kuendelea na taratibu zinazotakiwa kisheria na kikanuni na kuthibitisha kitengo cha Superdoll cha utoaji mafunzo kutambuliwa kama kituo maalum cha utoaji Mafunzo ya Umahiri.

