WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amemwagiza Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Iringa kufanya uchunguzi wa kina kuhusu ukusanyaji wa mapato ya maegesho katika eneo la Ifunda wilayani Iringa na kuwasilisha taarifa kamili kuhusu namna mapato hayo yalivyokuwa yakikusanywa kabla na baada ya mabadiliko ya mfumo wa ukusanyaji pamoja na matumizi yake.

Ametoa agizo hilo leo Jumamosi, Juni 6, 2026 wakati akizungumza na kusikiliza kero za wananchi wa Jimbo la Kalenga katika mkutano wa hadhara uliofanyika Ifunda wilayani Iringa mkoani Iringa.

Agizo hilo lilitolewa baada ya Waziri Mkuu kuwataka viongozi wa TANROADS, Halmashauri na TAKUKURU kutoa maelezo kuhusu mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya maegesho katika eneo hilo na mabadiliko yaliyofanyika katika usimamizi wake.

“Nataka ripoti yote ya zoezi la ukusanyaji jinsi ambavyo limefanyika, kabla na sasa. Nataka tujue fedha hizi zimeenda wapi na wahusika walikuwa nani,” alisema Dkt. Mwigulu.

Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kupitia mifumo ya uwajibikaji na maadili katika utumishi wa umma ili kuhakikisha maeneo yenye vishawishi vikubwa vya rushwa yanawekewa uangalizi unaostahili.

Amesema kuna umuhimu wa kuangalia upya mifumo ya matamko ya mali na maadili ili kuimarisha uwajibikaji kwa watumishi wanaosimamia maeneo yenye mikataba, leseni, makadirio ya kodi, madini, bandari na vyanzo vikubwa vya mapato ya Serikali.

“Tunataka ufuatiliaji mkubwa zaidi kwenye maeneo yenye vishawishi vikubwa vya rushwa. Lazima tuhakikishe rasilimali za umma zinawanufaisha Watanzania wote na si wachache wanaopata fursa ya kuzisimamia,” alisema.

Katika mkutano huo, Waziri Mkuu aliwataka watumishi wa umma kutambua kuwa nafasi walizonazo ni dhamana ya kuwatumikia wananchi na si kuwapa usumbufu wanapohitaji huduma.

“Ninapokuwa kwenye hizi ziara, nimekuwa ninawaambia watumishi wenzangu walioko maofisini kwamba kuwa kwenye hizi nafasi ni huduma, ni utumishi na kuwazungusha watu wanapotaka hizo huduma ni ushamba,” alisema.

Pia alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia utoaji wa haki kwa wananchi na kuchukua hatua dhidi ya watumishi watakaobainika kushindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo.

“Haki si hisani. Anayestahili haki apewe haki yake. Hatuwezi kuvumilia watu wanaocheza na haki za wananchi,” alisema.

Sambamba na hilo, Dkt. Mwigulu alieleza wasiwasi wake kuhusu malalamiko ya wananchi kuambiwa kununua dawa katika maduka binafsi wakati Serikali imeendelea kuwekeza fedha nyingi katika ununuzi wa dawa na vifaa tiba kwenye hospitali za umma.

“Hatuwezi kuwa na hospitali za umma kwa ajili ya kumuona daktari na kufanya vipimo tu, halafu dawa mwananchi akanunue mtaani. Kama kila siku wananchi wanaambiwa dawa hakuna, hizo dawa zilizo-expire zilitoka wapi?” alihoji.

Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuimarisha uwajibikaji, usimamizi wa rasilimali za umma na utoaji wa huduma bora kwa wananchi ili kuhakikisha maendeleo yanawanufaisha Watanzania wote kama ilivyokusudiwa.