Na Mwandishi Wetu, Arusha
MKURUGENZI wa Mauzo wa Turaco Collection Tanzania, Florenso Kirambata, amesema maonesho ya Karibu-KiliFAIR 2026 ni jukwaa muhimu la kuitangaza Tanzania kimataifa, kubadilishana uzoefu pamoja na kujenga ushirikiano wa kibiashara katika sekta ya utalii inayokua kwa kasi duniani.
Akizungumza wakati akiwasilisha hoteli za Turaco Collection katika maonesho hayo yanayofanyika jijini Arusha, Florenso alisema tukio hilo limekuwa likiwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya utalii, ukarimu, safari na uwekezaji kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali duniani.
Maonesho ya Karibu-KiliFAIR 2026 yanafanyika kuanzia Juni 4 hadi 7, 2026 katika Viwanja vya Magereza jijini Arusha.
Florenso alisema Turaco Collection imeendelea kuimarisha uwepo wake nchini kupitia hoteli zake zilizopo katika maeneo mbalimbali ya Tanzania. Alitaja hoteli hizo kuwa ni pamoja na Element by Westin Dar es Salaam na Delta Hotels by Marriott Dar es Salaam zilizopo Dar es Salaam.
Aidha, alisema Kaskazini mwa Tanzania kampuni hiyo inamiliki Turaco Ngorongoro Valley Lodge, Tribute Portfolio pamoja na Turaco Manyara View Lodge, Tribute Portfolio.
Kwa upande wa Zanzibar, alisema kampuni hiyo inamiliki Turaco Nungwi Resort, Tribute Portfolio, Turaco Spice Tree Stone Town, Tribute Portfolio pamoja na Beyt Al Salaam by Turaco.
Alieleza kuwa hoteli zote za Turaco Collection zinazobeba chapa za kimataifa zinaendeshwa kwa kuzingatia viwango vya Marriott International, hali inayochangia kuimarisha ubora wa huduma, matumizi ya teknolojia za kisasa na utoaji wa uzoefu wa kiwango cha kimataifa kwa wageni wanaotembelea Tanzania.
Akizungumzia matumizi ya Akili Bandia (AI) katika sekta ya ukarimu, Florenso alisema Marriott International inaamini teknolojia hiyo inapaswa kuboresha uzoefu wa wageni kwa kuufanya kuwa wa kibinafsi zaidi, wenye ufanisi mkubwa na rahisi, huku ikiendelea kudumisha misingi ya ukarimu unaozingatia mahusiano ya kibinadamu.
Alisema kampuni hiyo inaendelea kuwekeza katika teknolojia za AI ili kuboresha mifumo ya uwekaji nafasi za malazi, shughuli za uendeshaji wa hoteli, programu za uaminifu kwa wateja pamoja na huduma mbalimbali zinazotolewa kwa wageni.
“Teknolojia haitachukua nafasi ya ukarimu wa kibinadamu, bali itaongeza uwezo wa wafanyakazi wetu kutoa huduma bora zaidi. Mwelekeo wa Marriott International ni kutumia AI kuifanya safari ya mgeni, kuanzia kupanga safari, kuweka nafasi, kuwasili hotelini hadi kuondoka, kuwa rahisi, ya haraka na yenye uzoefu wa kipekee,” alisema Florenso.
Aliongeza kuwa kupitia ushirikiano wake na Marriott International, Turaco Collection inaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya teknolojia katika sekta ya ukarimu ili kuhakikisha wageni wanaotembelea Tanzania wanapata huduma zinazokidhi viwango vya kisasa vya kimataifa.

