Na Beda Msimbe, TBN Moscow.
Tanzania na Urusi zipo katika hatua za mwisho za majadiliano kuhusu mfumo wa matumizi ya fedha za ndani katika malipo ya biashara, hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kuongeza biashara kati ya mataifa hayo mawili.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliopo katika msafara wa ziara ya kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, nchini Urusi.
Profesa Mkumbo amesema kuwa Tanzania na Urusi zinatarajia kusaini hati za makubaliano hayo kabla ya kukamilika kwa ziara hiyo ya kihistoria.
Alisema kwa sasa kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili kinafikia Dola za Marekani milioni 200, na makubaliano hayo yatafungua ukurasa mpya wa ushirikiano wenye tija katika sekta za biashara, uwekezaji na maendeleo ya uchumi.
Aidha, Profesa Mkumbo alifafanua kuwa makubaliano hayo yatahusisha matumizi ya Shilingi ya Tanzania pamoja na sarafu ya Urusi katika mifumo ya malipo ya kibiashara ili kurahisisha miamala na kuongeza ufanisi wa biashara baina ya nchi hizo.
Alisema Urusi, ambayo ilitoa mchango mkubwa katika harakati za ukombozi wa kisiasa barani Afrika, sasa inaendelea kuwa mshirika muhimu katika ukombozi wa kiuchumi wa Tanzania kupitia uwekezaji, teknolojia na ushirikiano wa maendeleo.
Aliongeza kuwa Urusi imepiga hatua kubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, uchakataji wa mazao, uzalishaji wa mbegu bora na sekta ya madini, mambo ambayo yataisaidia Tanzania katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayotarajiwa kuanza kutumika Julai mwaka huu.
Profesa Mkumbo alisema moja ya mafanikio makubwa yanayotarajiwa kutokana na ziara hiyo ni kufanikisha ujenzi wa Reli ya Kusini kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Aidha, alisema Tanzania na Urusi zipo katika hatua za mwisho za makubaliano yatakayowezesha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuanzisha safari za moja kwa moja kati ya Dar es Salaam na Moscow, hatua itakayorahisisha usafiri, kukuza utalii na kuongeza fursa za biashara kati ya mataifa hayo mawili.
