Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Tanzania (VETA) zimesaini Hati ya Makubaliano (MoU) yenye lengo la kuwawezesha waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu kujifunza ujuzi mbalimbali wa kazi ili waweze kujitegemea na kurejea katika maisha ya kawaida.

Akizungumza leo Juni 04, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo, Kamishna Jenerali wa DCEA, , alisema ushirikiano huo ni hatua muhimu katika juhudi za Serikali za kuwasaidia waraibu waliomaliza tiba kujenga upya maisha yao.

Alisema tatizo la matumizi ya dawa za kulevya linaendelea kuathiri jamii nyingi duniani hususan vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa, huku madhara yake yakigusa afya, uchumi wa familia na kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu pamoja na kuporomoka kwa maadili katika jamii.

Kamishna Jenerali Lyimo alisema Serikali kupitia DCEA imekuwa ikiendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya ikiwemo kuzuia biashara haramu ya dawa hizo, kutoa elimu kwa jamii pamoja na kuimarisha huduma za tiba na urejeshaji kwa waraibu.

Alisema uzoefu unaonesha kuwa matibabu pekee hayatoshi ikiwa waraibu waliopona hawapati mazingira bora ya kurejea katika maisha ya kawaida kutokana na changamoto za ukosefu wa ajira, kipato na wakati mwingine kunyanyapaliwa na jamii.

“Changamoto hizi zinaweza kuwafanya baadhi yao kurejea tena kwenye matumizi ya dawa za kulevya, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuwapatia ujuzi na kuwawezesha kiuchumi,” alisema Lyimo.

Kupitia makubaliano hayo, waraibu waliopata nafuu watapata nafasi ya kujiunga na vyuo vya VETA nchini kwa gharama nafuu ili kujifunza taaluma mbalimbali zikiwemo ufundi seremala, umeme, ushonaji, ufundi magari, TEHAMA, upishi pamoja na stadi nyingine za kazi.

Aidha alisema matarajio ya DCEA ni kuona wahitimu hao wanapatiwa vifaa vidogo vya kuanzia kazi kulingana na taaluma walizosomea ili waweze kuanza shughuli za uzalishaji na kujipatia kipato halali.

Kamishna Jenerali Lyimo alisema DCEA itaendelea kushirikiana na taasisi za fedha zinazotoa mikopo midogomidogo ili kuwaunganisha wahitimu hao na fursa za mitaji kwa ajili ya kuanzisha biashara na shughuli nyingine za kiuchumi.

Alisema mpango huo ni utekelezaji wa dhana ya kuwapa watu nafasi ya pili maishani kwa kuwa waraibu waliopona wanahitaji kutiwa moyo, kuaminiwa na kuungwa mkono ili waweze kurejesha heshima yao katika jamii.

Pia aliishukuru VETA kwa kuona umuhimu wa mpango huo na kuamua kushirikiana na DCEA katika kusaidia kutatua changamoto za kijamii kupitia elimu ya ufundi stadi.

Vilevile aliwataka wadau mbalimbali wakiwemo sekta binafsi, mashirika ya kiraia, taasisi za kifedha na jamii kwa ujumla kushirikiana na Serikali katika kuwawezesha waraibu waliopona kupata ajira, elimu na mitaji ili waweze kuishi maisha yenye matumaini na mchango chanya kwa Taifa.

Alisema anaamini ushirikiano huo utakuwa chachu ya mabadiliko makubwa kwa maisha ya watu wengi pamoja na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.