Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Rais wa Shirikisho la Urusi Mhe. Vladmir Putin katika Ikulu ya Kremlin Jijini Moscow, tarehe 03 Juni, 2026.

…………

Na John Bukuku

Ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Shirikisho la Urusi imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili huku biashara, uwekezaji na miradi ya kimkakati vikipewa kipaumbele katika kuimarisha uchumi wa Tanzania.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, biashara kati ya Tanzania na Urusi imeonesha ukuaji mkubwa ambapo thamani ya biashara imeongezeka kutoka dola za Marekani milioni 178.8 mwaka 2020 hadi kufikia takribani dola milioni 307.5 mwaka 2025, hatua inayotafsiriwa kuwa mafanikio ya diplomasia ya uchumi inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita.

Kadhalika, mauzo ya bidhaa za Tanzania kwenda Urusi yameongezeka kwa kasi kutoka dola milioni 7.5 mwaka 2020 hadi dola milioni 29.5 mwaka 2025, jambo linaloonesha kuimarika kwa soko la bidhaa za Tanzania katika taifa hilo kubwa la Ulaya Mashariki.

Bidhaa zinazouzwa zaidi kutoka Tanzania kwenda Urusi ni pamoja na chai nyeusi, tumbaku, korosho, nazi, maua ya waridi, ngozi, madini pamoja na bidhaa za mapambo ya mbao, huku bidhaa hizo zikizidi kupata ushindani kutokana na ubora wake katika soko la kimataifa.

Kwa upande wa bidhaa zinazoingizwa kutoka Urusi kwenda Tanzania, nchi hiyo imeendelea kuwa chanzo muhimu cha pembejeo za viwandani ikiwemo mbolea, ngano, bidhaa za chuma, mafuta ya petroli, salfa pamoja na bidhaa mbalimbali zinazotumika katika uzalishaji wa viwanda na kilimo.

Ukuaji huo wa biashara unakwenda sambamba na ongezeko la uwekezaji wa miradi mikubwa inayotekelezwa na kampuni za Urusi nchini Tanzania ambapo hadi sasa zaidi ya miradi 70 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 434.22 imewekezwa katika sekta mbalimbali za uchumi.

Miradi hiyo imechangia kuzalisha zaidi ya ajira 3,018 kwa Watanzania huku ikifungua fursa mpya za maendeleo ya teknolojia, ujuzi na mapato ya ndani kupitia ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.

Mradi mkubwa zaidi unaovutia macho ya wawekezaji wa kimataifa ni Mradi wa Uranium wa Mkuju River uliopo Mkoa wa Ruvuma wenye thamani ya dola bilioni 1.2 unaotekelezwa na kampuni ya Mantra Tanzania Ltd ambayo ni tanzu ya kampuni ya ROSATOM ya Urusi.

Mradi huo unatarajiwa kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa uranium barani Afrika kwa uwezo wa kuzalisha hadi tani 3,000 za uranium kwa mwaka, huku Serikali ikitarajia kunufaika kupitia mapato, kodi na gawio la kila mwaka.

Hatua ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuzindua kiwanda cha majaribio cha uchakataji uranium katika eneo la Nyota mwaka 2025 imeelezwa kuwa ishara ya dhamira ya Tanzania kutumia rasilimali zake za madini kwa manufaa ya maendeleo ya taifa na kuongeza thamani ya sekta ya madini nchini.

Mbali na mradi wa uranium, Tanzania na Urusi pia zimeendelea kushirikiana katika sekta ya nishati kupitia miradi ya gesi asilia na CNG inayotekelezwa kwa ubia kati ya Gazprom International na kampuni ya Anric Energy, hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa nishati safi na nafuu nchini.

Katika sekta ya usafirishaji na bandari, kampuni ya FESCO kupitia ushirikiano wake na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inaendelea na mipango ya kuboresha miundombinu ya Bandari ya Dar es Salaam ikiwemo upembuzi yakinifu wa maendeleo ya gati namba 14 na 15 ili kuongeza uwezo wa bandari hiyo kuhudumia mizigo zaidi ya tani milioni 30 kwa mwaka.

 Ziara ya Rais Samia nchini Urusi inaweza kuwa chachu ya kuvutia uwekezaji mpya, kuongeza biashara ya kimataifa na kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha biashara, nishati na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.