NA DENIS MLOWE IRINGA
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, ametoa wito kwa wadau wa sekta ya mifugo kuongeza juhudi katika kuimarisha uzalishaji, usindikaji na matumizi ya maziwa nchini ili kukuza uchumi wa wafugaji na kuhakikisha usalama wa chakula.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Wiki ya 29 ya Maadhimisho ya wiki ya  Maziwa yaliyofanyika katika Uwanja wa Mwembetogwa mkoani Iringa, Waziri Bashiru alisema maendeleo ya sekta ya maziwa yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, Bunge, taasisi za mifugo na wadau mbalimbali.

Alisema ni muhimu kufanya tathmini ya hatua zilizofikiwa katika sekta hiyo pamoja na kuweka mikakati ya kufikia malengo mapya ya uzalishaji na usindikaji wa maziwa.

Waziri Bashiru alieleza kuwa baadhi ya viwanda vya usindikaji maziwa vinakabiliwa na changamoto za kifedha na usimamizi, hali inayosababisha wafugaji kushindwa kupata malipo kwa wakati licha ya kuuza maziwa yao.

Alitolea mfano wa Kiwanda cha Tanga Fresh, akisema kinahitaji maboresho ya kiutendaji na kifedha ili kiweze kutoa huduma bora kwa wafugaji na kuchangia kikamilifu katika ukuaji wa sekta hiyo.

Aidha, aliwataka wadau kutumia teknolojia za kisasa kuhamasisha wananchi kunywa maziwa na kuelewa umuhimu wake katika lishe bora, hususan kwa watoto.

“Teknolojia inaweza kutumika kama chombo cha kuhamasisha matumizi ya maziwa na kubadili mtazamo wa jamii kuhusu umuhimu wa bidhaa za mifugo,” alisema.

Waziri Balozi Dkt Bashiru  aisisitiza umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa maziwa ili kukidhi mahitaji ya viwanda vya usindikaji.

Alisema baadhi ya wawekezaji wamewekeza katika mitambo ya kisasa ya kutengeneza maziwa ya unga, lakini changamoto kubwa bado ni upatikanaji wa maziwa ya kutosha kwa ajili ya uzalishaji.

Alibainisha kuwa teknolojia ya usindikaji wa maziwa ya unga ina faida kubwa kwa kuwa huongeza muda wa kuhifadhi maziwa, kurahisisha usafirishaji na kupunguza upotevu wa maziwa kwa wafugaji.

Waziri Bashiru alieleza kuwa Tanzania bado ina nafasi kubwa ya kuongeza uzalishaji wa maziwa ikilinganishwa na baadhi ya nchi jirani ambazo zimepiga hatua kubwa katika sekta hiyo.

Katika hatua nyingine, aliagiza taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushiriki kikamilifu katika maonesho mbalimbali ya kitaifa, hususan Maonesho ya Nane Nane, kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma na fursa zilizopo katika sekta ya mifugo na uvuvi.

Alisema mabanda ya wizara na taasisi zake yanapaswa kuwa vituo vya elimu, ushauri na kupokea maoni ya wananchi badala ya kuwa sehemu za maonesho pekee.

Pia aliwashukuru wadau mbalimbali walioshiriki kufanikisha maadhimisho hayo, akiwemo Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Shirika la Uwekezaji la UTT pamoja na taasisi nyingine za umma na binafsi zinazochangia maendeleo ya sekta ya maziwa nchini.

Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha uzalishaji, usindikaji na matumizi ya maziwa pamoja na kuonyesha mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.