……………
NA DENIS MLOWE, IRINGA 
MRATIBU wa Mradi wa Climate-Smart Dairy Transformation Project (C-SDTP), Razalo Kapera, amesema mradi huo unaendelea kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya maziwa nchini kwa lengo la kuongeza uzalishaji, kuboresha kipato cha wafugaji wadogo na kuimarisha uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kapera amezungumza hayo katika Kongamano la Wadau wa Tasnia ya Maziwa 2026 lililofanyika katika Ukumbi wa Royal Palm mkoani Iringa, ambapo wadau mbalimbali wa sekta ya maziwa kutoka serikalini, taasisi za maendeleo, sekta binafsi na wafugaji walikutana kujadili maendeleo na mustakabali wa sekta hiyo nchini.
Amesema mradi huo unatekelezwa katika halmashauri 21 za Tanzania Bara pamoja na maeneo matano ya Zanzibar, hivyo kufikisha jumla ya maeneo 26 ya utekelezaji. Kwa mujibu wa Kapera, Mkoa wa Mbeya unatekeleza mradi katika Halmashauri za Busokelo, Rungwe na Mbeya DC, huku Mkoa wa Njombe ukiwa na Halmashauri za Njombe DC na Wanging’ombe.
Ameongeza kuwa Mkoa wa Iringa unahusisha Halmashauri za Iringa DC, Kilolo na Mufindi, Mkoa wa Morogoro ukiwa na Mlimba, Mvomero na Kilosa. Mkoa wa Pwani unatekeleza mradi kupitia Halmashauri za Rufiji na Mkuranga, wakati Mkoa wa Tanga ukiwa na Mkinga, Muheza na Handeni.
Kwa upande wa Mkoa wa Kilimanjaro, mradi unatekelezwa katika Halmashauri za Siha na Moshi DC, huku Mkoa wa Arusha ukiwa na Meru DC na Arusha DC.
“Maeneo haya ni makubwa sana na yanahitaji mfumo madhubuti wa uratibu ili kuhakikisha malengo ya mradi yanafikiwa kwa ufanisi. Kutokana na idadi ndogo ya watumishi wa mradi ngazi ya wizara ukilinganisha na ukubwa wa maeneo ya utekelezaji, tumeshirikiana kwa karibu na Ofisi ya Rais – TAMISEMI katika kuratibu shughuli zote za mradi,” amesema Kapera.
Amesema kupitia ushirikiano huo, waratibu wa mradi wameteuliwa katika ngazi za mikoa ili kusimamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali, kufuatilia maendeleo na kuhakikisha mawasiliano kati ya mradi, serikali za mitaa na wadau wengine yanaimarishwa.
Kapera amesema waratibu hao wamekuwa na mchango mkubwa katika kuwatambua wanufaika wa mradi, kuratibu shughuli za maendeleo na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinawafikia walengwa kwa wakati.
Akizungumzia mipango ya kuboresha sekta ya mifugo, Kapera amesema mradi umepanga kusambaza mbuzi 8,600 kwa wanufaika katika maeneo mbalimbali ya utekelezaji.
“Kati ya mbuzi hao, asilimia 20 watatolewa kwa kaya maskini kupitia mfumo wa ruzuku, ambapo wanufaika hawatatakiwa kurejesha gharama yoyote. Asilimia 80 iliyobaki itasimamiwa kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), na taratibu za utekelezaji wake zinaendelea kukamilishwa,” amesema.
Kapera amesema pamoja na hatua hizo, mradi umejipanga kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo katika mwaka wa fedha 2026/2027 baada ya kukamilisha maandalizi ya msingi yaliyofanyika katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji.
Ameeleza kuwa mwaka wa kwanza ulikuwa wa kuandaa mifumo ya usimamizi, kujenga uwezo wa timu za utekelezaji na kuweka misingi ya uratibu wa shughuli za mradi katika maeneo yote yanayonufaika.
“Kwa sasa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 imeidhinishwa na tunaelekeza nguvu kubwa katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo zenye matokeo ya moja kwa moja kwa wafugaji,” amesema.
Kapera amesema kipaumbele kikubwa katika mwaka huo kitakuwa kuboresha malisho ya mifugo ili kuongeza uzalishaji na tija katika sekta ya maziwa. Aidha, mradi utawekeza katika kuboresha na kuimarisha vituo vya kukusanyia maziwa ili kuongeza thamani ya mazao ya wafugaji na kuboresha upatikanaji wa masoko.
Ameongeza kuwa mafanikio ya uwekezaji huo yatategemea pia uimara wa vikundi vya wafugaji, hivyo mradi utaendelea kuimarisha uwezo wa Producer Organizations ili viweze kusimamia shughuli za uzalishaji, ukusanyaji na uuzaji wa maziwa kwa ufanisi zaidi.
“Lengo letu ni kuhakikisha wafugaji wanapata huduma bora za mifugo, malisho yenye tija, masoko yenye uhakika na fursa za kuongeza kipato. Tunataka kuona sekta ya maziwa inakuwa ya kisasa, yenye ushindani na inayochangia kwa kiwango kikubwa katika maendeleo ya uchumi wa taifa na ustawi wa wananchi,” amesema Kapera.
Mradi wa C-SDTP unafadhiliwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania, Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Heifer International, Agence Française de Développement (AFD), OPEC Fund pamoja na wadau wengine wa maendeleo, ukiwa na dhamira ya kuimarisha mnyororo wa thamani wa maziwa na kuboresha maisha ya maelfu ya wafugaji wadogo nchini.