WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba leo (Jumamosi, Mei 30, 2026) akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Singida amekagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Huduma ya Maji wa Mji wa Manyoni unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 28 na unaotarajiwa kuhudumia wakazi zaidi ya 64,667.

Akipokea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Manyoni (MAUWASA), Mhandisi Lucas Mwinuka, Dkt. Mwigulu alielezwa kuwa mradi huo umefikia asilimia 80 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika Agosti 10, 2026.

Mhandisi Mwinuka alisema mradi huo unatekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Maji na unahusisha uchimbaji wa visima vya maji, ujenzi wa kituo cha kusukuma maji, ujenzi wa tanki lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni mbili za maji pamoja na ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji kwa wananchi.

Alisema mradi huo utakapokamilika utaongeza uzalishaji wa maji kutoka wastani wa lita milioni 2.057 kwa siku hadi lita milioni 6.48 kwa siku na hivyo kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi zaidi ya 64,667 wa mji wa Manyoni.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Andrea Mathew alisema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.

Mhandisi Kundo alisema mradi wa Manyoni ni sehemu ya kifurushi cha nne cha Mradi wa Miji 28 unaotekelezwa katika miji ya Kiomboi, Singida, Manyoni, Chamwino, Chemba na Mugumu kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 142. Alisema kukamilika kwa miradi hiyo kutaimarisha upatikanaji wa maji safi na salama, kuchochea shughuli za kiuchumi na kuimarisha ustawi wa wananchi katika maeneo hayo.

Alisema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuongeza upatikanaji wa maji katika Mji wa Manyoni kutoka asilimia 49 ya sasa hadi asilimia 100 na kuweka msingi wa kukidhi mahitaji ya maji kwa zaidi ya miaka 20 ijayo kutokana na ukuaji wa mji na ongezeko la idadi ya watu.

Aidha, alisema Serikali imeanza hatua za kuhifadhi maeneo ya vyanzo vya maji ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa huduma hiyo sambamba na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.