Wakubaliana kuimarisha masuala ya kilimo, nishati na usalama
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amekutana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Congo, Anatole Collinet Makosso na kujadiliana naye masuala ya kidiplomasia ikiwemo usalama, mazingira, kilimo na nishati kwenye kikao kilichofanyika ofisini kwa mwenyeji wake, Boulevard Alfred Raoul, Brazzaville, jijini Brazzaville.
Akizungumza na mwenyeji wake leo (Jumatano, Mei 27, 2026) Dkt. Mwigulu amesema mbali na kupata fursa ya kushirki mkutano wa mwaka wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), ziara yake nchini Congo ni ya kukuza mahusiano baina ya nchi hizo mbili.
“Ujio wetu nchini Congo Brazzaville, umelenga kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia lakini pia kuhimiza haja ya nchi zetu kukuza ushirikiano wa kikanda, kutunza utulivu, amani na maendeleo ya bara la Afrika.”
Alimwelezea mikakati ambayo Dkt. Samia ameiweka katika kukuza kilimo kupitia njia ya umwagiliaji, kukuza uchumi kupitia sekta ya utalii na suala zima la uhifadhi wa mazingira.
Waziri Mkuu pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Congo, Denis Sassou-Nguesso kwa kumualika Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kushiriki mkutano huo ambao ilimpendeza kumtuma yeye amuwakilishe.
Ametumia fursa hiyo kufikisha ujumbe wa Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan wa kuiomba nchi ya Congo imuunge mkono mgombea wa Tanzania kwenye nafasi ya Jaji wa Mahakama ya Kimataifa (ICC), Dkt. Deo John Nangela ambaye uchaguzi wake umepangwa kufanyika Desemba, mwaka huu jijini New York, Marekani.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Congo alimshukuru Dkt. Mwigulu kwa kushiriki mkutano huo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye alisema anatambua kwamba ana majukumu mengine ya kitaifa.
Alisema nchi hiyo ina mengi ya kujifunza kutoka Tanzania hasa kwenye sekta ya nishati. “Ninajua kwamba hakuna maendeleo bila uwepo wa umeme au nishati. Na nchi ya Tanzania iliitisha mkutano mkubwa wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati ujulikanao ‘misheni 300’ ambao unalenga kuhakikisha wananchi milioni 300 barani Afrika wanapata umeme ifikapo mwaka 2030. Tunapaswa tuungane kutafuta fedha za kuendeleza mradi huu,” alisisitiza.
Alisema nchi yake inahimiza utunzaji wa mazingira na ingependa kuona suala la uendelezaji wa Bonde la Mto Congo linapewa uzito mkubwa kwa faida ya vizazi vijavyo. Alisema nchi hiyo pia inaendeleza uchumi wa bluu.
Mawaziri wakuu hao walikubalina kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa Congo pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Congo wahakikishe wanaitisha Tume ya Kudumu ya Ushirikiano wa Pamoja ili kuhakikisha maelekezo yao yanafanyiwa kazi.
