Na Atley Kuni, WAF – Nkinga Tabora
Wataalamu wa afya kutoka Wizara ya Afya pamoja na wadau wa mapambano dhidi ya fistula wamehimizwa kuimarisha huduma hadi ngazi ya jamii ili kuongeza kasi ya kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.
Rai hiyo imetolewa Mei 21, 2026 mkoani Tabora na Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Boniface Marwa, wakati wa kongamano linaloendelea katika Hospitali ya Rufaa Maalum ya Nkinga kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Fistula Duniani yatakayofanyika Mei 23, 2026.
Dkt. Marwa amesema licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali, bado baadhi ya wanawake wanaendelea kupata fistula kutokana na changamoto za kijamii, kiuchumi na ucheleweshaji wa kupata huduma za afya wakati wa ujauzito na kujifungua.
Amesema uwepo wa visa vya fistula unaonyesha umuhimu wa kuongeza elimu kwa jamii, kuimarisha huduma za afya ya uzazi na kuhakikisha wajawazito wanapata huduma mapema katika vituo vya afya.
Aidha, amesisitiza kuwa wataalamu wa afya ngazi ya jamii wanapaswa kupewa nafasi kubwa zaidi ya kutoa elimu kuhusu fistula, kwani bado uelewa kuhusu tatizo hilo ni mdogo katika jamii nyingi.
Kwa upande wake, Mratibu wa Huduma za Fistula kutoka Wizara ya Afya, Bi. Fidea Obimbo, amesema Serikali inaendelea kuimarisha afua za mapambano dhidi ya fistula kwa kushirikiana na chama cha wataalamu wa afya wanaoshughulikia huduma hizo.
Amesema mikakati inayotekelezwa inalenga kufanikisha malengo ya kitaifa na ya kimataifa ya kutokomeza fistula kupitia sera ya afya inayosisitiza uboreshaji wa huduma za afya ya mama na mtoto.
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Fistula Duniani mwaka huu yatafanyika mkoani Tabora chini ya kaulimbiu isemayo: “Afya ni haki ya msingi ya kila mwanamke; wekeza kutokomeza fistula na majeraha yatokanayo na uzazi,” huku lengo kuu likiwa ni kutokomeza kabisa ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.

