Na. Ssgt Mawazo Mtondo – Dodoma.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeendelea kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai kwa kutoa mafunzo ya Mfumo wa upimaji wa utendaji kazi kwa Maafisa na Askari wa Vyombo vya Usalama vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi (Security Organs Performance Management Information System – SOPMIS). Mafunzo hayo yanatolewa kwa Maafisa na Askari wakufunzi (TOTs) kutoka vyombo vilivyo chini ya Wizara hiyo ili kuwawezesha washiriki kutoa mafunzo kwa watumishi wenzao juu ya matumizi sahihi ya mfumo tajwa.
Mafunzo hayo yanafanyika kwa siku saba kuanzia Mei 20-27, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji uliopo jijini Dodoma, yakihusisha washiriki kutoka Vyombo vya Usalama vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Vyombo vinavyonufaika na Mafunzo ya Mfumo huo ni pamoja na Jeshi la Polisi Tanzania (TPF), Jeshi la Magereza Tanzania (TPS), Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (FRF) pamoja na Idara ya Uhamiaji (TISD).
Aidha, Mfumo huo unatarajiwa kuongeza uwazi wa upimji wa utendaji kazi kwa watumishi wa vyombo hivyo, ikiwa ni pamoja na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu bila kuathiri Usalama wa taarifa zinazotumika.
Pamoja na mambo mengine washiriki wa Mafunzo hayo watajifunza jinsi ya kupanga, kutekeleza, kufuatilia na kutathmani utendaji kazi wa Mfumo huo.
Kupitia matumizi ya Mfumo wa e-Utendaji, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inalenga kuimarisha uwajibikaji, kuboresha usimamizi wa rasilimali watu na kuhakikisha utekelezaji bora wa malengo ya Taasisi zake kwa kuzingatia matumizi ya teknolojia ya kisasa.

