Na John Bukuku, Dar es Salaam

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) imetoa tahadhari kwa wananchi kuhusu uwepo wa dawa ya binadamu isiyosajiliwa inayojulikana kwa jina la VEGA-100 Tablets ambayo imekuwa ikiingizwa na kuuzwa kiholela katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMDA, dawa hiyo imekuwa ikikamatwa mara kwa mara kupitia ukaguzi na operesheni maalum zinazofanywa na mamlaka hiyo katika soko la dawa nchini.

TMDA imesema uchunguzi wake umebaini kuwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wanajihusisha na usambazaji pamoja na uuzaji wa dawa hiyo licha ya kutokuwa na usajili wa matumizi hapa nchini.

Dawa hiyo yenye kiambata hai cha Sildenafil Citrate, imeelezwa kuwa hutumika kuongeza nguvu za kiume kwa wanaume wenye changamoto ya kutosimamisha uume wakati wa tendo la ndoa. Aidha, jina la mtengenezaji linaloonekana kwenye lebo za dawa hiyo ni Signature Pharmaceuticals Ltd ya nchini India.

Mamlaka hiyo imeonya kuwa matumizi holela ya dawa hiyo yanaweza kusababisha madhara makubwa kiafya ikiwemo kushuka kwa shinikizo la damu, kupoteza uwezo wa kuona au kusikia ghafla pamoja na uume kubaki umesimama kwa muda mrefu zaidi ya saa nne.

Madhara mengine yaliyotajwa ni pamoja na maumivu ya kichwa, kuona maluelue, pua kujaa makamasi, kiungulia, kushindwa kumeng’enya chakula vizuri na maumivu ya misuli au mgongo.

TMDA imesisitiza kuwa dawa hiyo haifai kutumiwa kwa kuwa ubora, usalama na ufanisi wake haujathibitishwa kutokana na kutosajiliwa rasmi na mamlaka hiyo.

Kutokana na hali hiyo, TMDA imewataka wananchi kutoa taarifa kuhusu watu au kampuni zinazojihusisha na usambazaji wa dawa hiyo ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika kwa mujibu wa sheria.

Wananchi wametakiwa kutoa taarifa kwenye vituo vya Polisi vilivyo karibu nao au katika ofisi za TMDA zilizopo Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Ruvuma, Tabora na Geita. Pia taarifa zinaweza kutumwa kupitia barua pepe ya TMDA au simu ya bure ya mamlaka hiyo.

Aidha, wananchi wameaswa kutotumia dawa bila ushauri wa madaktari, wafamasia au wataalam wengine wa afya wakikumbushwa kuwa dawa ni kemikali zenye uwezo wa kusababisha madhara makubwa hata vifo iwapo zitatumika vibaya.

TMDA imehimiza ushirikiano wa jamii katika mapambano dhidi ya dawa bandia, duni na ambazo hazijasajiliwa ili kulinda afya za wananchi.