Na Mwandishi Wetu

WAKATI mataifa mengi ya Afrika yaliyo Kusini mwa Jangwa la Sahara yakishuhudia kasi kubwa ya ukuaji wa miji, Tanzania imechukua msimamo thabiti wa kudhibiti uendelezaji holela wa makazi pembezoni mwa miji ili kuepuka gharama kubwa za kurekebisha miundombinu baadaye.

Akizungumza katika Jukwaa la 13 la Miji Duniani (WUF13) jijini Cairo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, ameeleza kuwa Tanzania imeweka mkakati madhubuti wa kitaifa wa kusuka upya mustakabali wa miji kabla ya ujenzi holela kushamiri.

Prof. Shemdoe amesema kuwa serikali imeamua kuelekeza nguvu zake katika maeneo ya pembezoni mwa miji, akibainisha kuwa Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Mbeya na Arusha zinapanuka kwa kasi ya mlalo.

Ameonya kuwa ukuaji wa miji bila mpango wa mapema unasababisha makazi yasiyo rasmi, ukosefu wa ajira na changamoto za huduma muhimu kama maji safi, umeme na usafi wa mazingira.
“Ukuaji wa miji unapotokea bila mipango ya mapema unatengeneza makazi yaliyotawanyika na ukosefu wa ajira.

Kuweka miundombinu katika maeneo haya baada ya kuwa tayari yamejengwa ni gharama kubwa zaidi kuliko kuyapanga mapema kabla hayajajengwa,” amesema Prof. Shemdoe.
Serikali imezindua miongozo mipya ya mipango ya miji na udhibiti wa uendelezaji, pamoja na miongozo ya kuhifadhi mazingira ya kijani.

Kupitia mifumo ya kidijitali na taarifa za kijiografia (GIS), serikali inarasimisha makazi ya pembezoni na kugawa viwanja vilivyopimwa ili kuhakikisha matumizi bora ya ardhi.

Prof. Shemdoe ametaja Programu ya Tanzania ya Kupandisha Kiwango cha Miundombinu na Ushindani wa Miji (TACTIC) inayotekelezwa katika miji 45, ikilenga barabara, masoko na udhibiti wa mafuriko.

Aidha, ameeleza kuwa Mradi wa Maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP) Awamu ya Kwanza na ya Pili unalenga kuongeza miundombinu inayohimili mabadiliko ya tabianchi.
Serikali pia inawekeza katika miji ya kati na pembezoni kwa kujenga masoko ya kisasa 28, vituo vya usindikaji wa mazao ya kilimo na kuanzisha Ukanda wa Kiuchumi wa Kwala.

Hatua hizi zinahakikisha fursa za ajira zinapatikana karibu na wananchi na kupunguza shinikizo la ukuaji holela katika Dar es Salaam.

Prof. Shemdoe amesisitiza kuwa ujenzi wa masoko makubwa zaidi ya 15 na uboreshaji wa sekta isio rasmi, hususan kwa vijana na wafanyabiashara wadogo ni sehemu ya ajenda kuu ya kitaifa ya kupunguza tatizo la ajira na kuimarisha uchumi wa miji.

Kwa mkakati huu, Tanzania inalenga kujenga miji yenye usawa, yenye miundombinu imara na inayoweza kukabiliana na changamoto za tabianchi, huku ikiepuka gharama kubwa za kurekebisha makosa ya uendelezaji holela.