*Serikali yaja na mkakati wa kuongeza uzalishaji, kutoa mizinga 11,000

Tabora, Mei 21, 2026

Sekta ya ufugaji nyuki nchini imepata msukumo mpya baada ya Serikali kutangaza mpango wa kutoa mizinga 11,000 pamoja na mafunzo kwa zaidi ya wafugaji 3,000 katika mwaka wa fedha 2026/2027, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji wa asali na kuinua uchumi wa wananchi wanaotegemea shughuli hiyo.

Hatua hiyo ilibainishwa katika mdahalo mkubwa wa wadau wa sekta ya nyuki uliofanyika mkoani Tabora, ukihusisha wafugaji wa nyuki, wataalamu wa misitu na nyuki, taasisi mbalimbali pamoja na wadau wa maendeleo kujadili mikakati ya kuimarisha ufugaji wa kisasa na kuongeza thamani ya mazao ya nyuki nchini.

Akizungumza katika mdahalo huo, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Bi. Upendo Joseph Haule, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, alisema ufugaji wa nyuki umeendelea kuwa chanzo muhimu cha ajira na kipato kwa wananchi wengi, hasa wanaoishi jirani na maeneo ya misitu.

Alisema Serikali inaendelea kuhimiza matumizi ya teknolojia bora, mizinga ya kisasa na uwekezaji katika uchakataji wa mazao ya nyuki ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la kimataifa.

“ Mkoa umeendelea kuhamasisha uwekezaji katika uchakataji wa mazao ya nyuki, matumizi ya teknolojia bora pamoja na kuongeza thamani ya bidhaa za nyuki. Pia umeanzishwa wazo la kuunda Kongani la Ushindani wa Asali ya Tabora (Tabora Honey Competitive Cluster),” alisema Bi. Haule.

Alisema lengo la kongamano hilo ni kuwakutanisha wadau wote wa mnyororo wa thamani wa mazao ya nyuki ili kuongeza ubora na ushindani wa asali ya Tabora katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Bi. Haule alionya kuhusu ongezeko la matukio ya moto wa misitu yanayohatarisha shughuli za ufugaji nyuki katika baadhi ya maeneo na kusisitiza umuhimu wa jamii kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya chakula vya nyuki.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki Wizara ya Maliasili na Utalii Bw, Daniel Pancrasi, alisema katika mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali imetoa jumla ya mizinga 9,215 na kuwafikia wafugaji 4,934 kupitia mafunzo mbalimbali ya ufugaji wa kisasa wa nyuki.

Alisema katika mwaka ujao wa fedha, Serikali inalenga kuongeza utoaji wa mizinga hadi 11,000 sambamba na kuendelea kuwajengea uwezo wananchi ili sekta hiyo iwe chanzo kikubwa cha mapato ya kaya na taifa.

“Tunawaomba wananchi kuchangamkia fursa hii kwa kuingia kwenye ufugaji wa kisasa wa nyuki ambao una tija kubwa kiuchumi na kimazingira,” alisema Bw. Pancras.

Katika mdahalo huo, wadau walisisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya mazao ya nyuki kupitia usindikaji wa kisasa, ufungashaji bora na kuzingatia viwango vya ubora vinavyokubalika kimataifa ili bidhaa za Tanzania ziweze kushindana kwenye masoko ya nje.

Pia walipendekeza kuongezwa kwa mafunzo kwa vikundi vya wafugaji wa nyuki, hususan vijana na wanawake, ili waweze kushiriki kikamilifu katika uzalishaji, usindikaji na biashara ya mazao ya nyuki.

Wadau hao walieleza kuwa sekta ya nyuki ina uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira, kuongeza mapato ya wananchi na kuchangia uhifadhi wa misitu, endapo uwekezaji wa kimkakati utaongezwa na ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na jamii utaimarishwa.