Mbunge wa Jimbo la Hai, Saashisha Mafuwe, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo, akieleza kuwa wananchi wamemtuma kutoa shukrani zao kutokana na kazi kubwa zinazofanyika.

Ametoa pongezi hizo leo Alhamisi Mei 21, 2026 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi. 

 

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo, Mafuwe amesema Wizara ya Ujenzi imefanya kazi kubwa ikiwemo ujenzi wa kalvati (daraja dogo) katika eneo la KIA pamoja na uwekaji wa taa za barabarani ambazo zimeongeza usalama na kurahisisha usafiri kwa wananchi.

 

“Sio tu tunasifu na kushukuru, bali tunafanya hivyo kwa kutaja vitu vilivyofanyika. Kalvati limejengwa na taa za barabarani zimefungwa,” 

 

alisema Mafuwe.

Aidha, amesema katika eneo la Bomang’ombe Serikali imeweka taa za kuongozea magari, jambo ambalo amesema halijawahi kutokea kwa muda mrefu.

 

“Pale Bomang’ombe umeweka taa za kuongozea magari, tangu dunia imeumbwa taa hizo hazikuwepo ila sasa zimewekwa. Kwanini tusimfie Rais Samia, huo ndio uungwana,” aliongeza.

 

Mbunge huyo pia 

amempongeza Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, kwa usimamizi wa miradi mbalimbali ya miundombinu ndani ya jimbo hilo, ikiwemo ujenzi wa Daraja la Mkowa ambalo linaendelea kukamilishwa pamoja na Daraja la Kikafu.

Mbali na hilo, Mafuwe amesema katika bajeti ya Wizara ya Ujenzi kuna miradi mingi iliyoainishwa kwa ajili ya Jimbo la Hai, ikiwemo mradi wa barabara ya Sadala kwenda Lemira yenye urefu wa kilomita 16, hatua ambayo itaongeza maendeleo ya uchumi na kurahisisha huduma za usafiri kwa wananchi wa eneo hilo.