Na Mwandishi wetu Kibondo

Mahakama ya Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma imemtia hatiani Fundi Sanifu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Kibondo, Bw. Felix Julius Mwara (33), kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka.

Hukumu hiyo ilitolewa katika shauri la uhujumu uchumi namba ECC 4485/2026 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kibondo, Mheshimiwa Maira M. Makonya.

Kwa mujibu wa taarifa ya TAKUKURU Wilaya ya Kibondo, mshtakiwa alikutwa na hatia ya kosa la matumizi mabaya ya madaraka kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329 marejeo ya mwaka 2022, kikisomwa pamoja na Aya ya 21 ya Jedwali la Kwanza pamoja na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupanga, Sura ya 200 marejeo ya mwaka 2022.

Mahakama ilimtaka mshtakiwa kulipa faini ya Shilingi milioni 3.5, ambapo amelipa na kuachiwa huru.

Ilielezwa mahakamani kuwa mnamo Machi 4, 2024, Bw. Mwara aliomba zabuni kupitia kampuni yake ya Kirangita Investment kutoka Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Kibondo Mjini (KIUWASA) kwa ajili ya mradi wa kuhamisha vifaa vya miundombinu ya maji kupisha ujenzi wa barabara mpya ya Kibondo kwenda Mabamba.

Mshtakiwa alifanikiwa kushinda zabuni hiyo yenye thamani ya Shilingi milioni 33.6 kupitia kampuni yake binafsi.

Hata hivyo, ilidaiwa kuwa kitendo hicho kilikuwa kinyume na Kanuni ya 81(1)(b) ya Kanuni za Manunuzi ya Umma za mwaka 2013, kama ilivyotangazwa katika Tangazo la Serikali Na. 416 la Desemba 20, 2013, kutokana na kushindwa kuweka wazi maslahi aliyokuwa nayo katika kampuni iliyopata zabuni hiyo.

Aidha, ilielezwa kuwa Bw. Mwara alikuwa mmiliki wa kampuni hiyo na wakati huo huo alikuwa mjumbe wa Kamati ya Mapokezi na Ukaguzi pamoja na Msimamizi Mkuu wa mradi huo kwa niaba ya KIUWASA.

Shauri hilo liliendeshwa na waendesha mashitaka wa TAKUKURU, Bw. Davis Junior na Bw. Agustino Lohay.

TAKUKURU Wilaya ya Kibondo imesema itaendelea kusimamia uwajibikaji na kupambana na vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka katika utekelezaji wa miradi ya umma.