Asisitiza ushirikiano wa kikanda katika kulinda rasilimali za ziwa

Aagiza kuimarishwa kwa mifumo ya uokoaji na usalama majini_

Ataka matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa rasilimali za maji_

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinapaswa kuendelea kushirikiana kulinda na kulihifadhi Ziwa Victoria kwa kuwa ni rasilimali muhimu inayogusa maisha, uchumi na mustakabali wa mamilioni ya wananchi wa ukanda huo.

“Ziwa Victoria si mali ya nchi moja pekee. Ni rasilimali inayotuunganisha kama Jumuiya na tunapaswa kushirikiana katika kulinda mazingira, usalama na uchumi unaotegemea ziwa hili,” amesema Dkt. Nchemba.

Amesema hayo leo Alhamisi, Mei 21, 2026 wakati akizindua rasmi Siku ya Ziwa Victoria na kufunga kilele cha maadhimisho ya kwanza yaliyofanyika katika Viwanja vya Nanenane Nyamhongolo jijini Mwanza.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ilikuwa “Maji Yetu, Mustakabali Wetu: Tuungane kwa Uendelevu wa Bonde la Ziwa Victoria.”

Katika hotuba yake, Waziri Mkuu amesema maadhimisho hayo yanapaswa kuwa sehemu ya kuhamasisha usimamizi endelevu wa rasilimali za maji, kuimarisha mshikamano wa kikanda na kuongeza uwajibikaji wa pamoja katika kulinda mazingira ya Ziwa Victoria.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kuimarisha mifumo ya usalama majini, kudhibiti uharibifu wa mazingira na kuendeleza matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa rasilimali za ziwa hilo.

“Sote tunawajibika kutunza mazingira ya Ziwa Victoria kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa mifumo ya uokoaji majini pamoja na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kufuatilia shughuli za uvuvi, ubora wa maji na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Pia ametoa wito kwa taasisi za utafiti kuendelea kufanya tafiti zitakazosaidia kupata suluhisho la changamoto mbalimbali zinazoathiri mazingira ya Ziwa Victoria ikiwemo ongezeko la magugu maji na uharibifu wa vyanzo vya maji.

Awali, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema Tanzania itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kuhifadhi Ziwa Victoria kwa kuwa ni nguzo muhimu ya uchumi, usalama na maendeleo ya wananchi wa ukanda wa ziwa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Ole Millya amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kuandaa na kutekeleza mipango ya pamoja ya kuhifadhi rasilimali za Bonde la Ziwa Victoria.

Naye Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria, Masinde Bwire amesema maadhimisho hayo ni hatua muhimu ya kuimarisha dhamira ya pamoja ya nchi wanachama katika kulinda moja ya rasilimali kubwa za maji barani Afrika.

Wawakilishi kutoka Kenya na Uganda waliishukuru Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kukabiliana na changamoto za uchafuzi wa mazingira, mabadiliko ya tabianchi na usalama wa majini ndani ya Ziwa Victoria.

Katika maadhimisho hayo, Waziri Mkuu pia alizindua rasmi Siku ya Ziwa Victoria ambayo sasa itaadhimishwa kila mwaka tarehe 21 Mei katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.