Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewataka wananchi kuchukua tahadhari kufuatia matarajio ya upepo mkali wenye kasi ya hadi kilomita 40 kwa saa katika baadhi ya maeneo ya pwani nchini kwa siku tano kuanzia leo.
Mikoa inayotarajiwa kuathirika ni Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Lindi na Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Kwa mujibu wa TMA, hali hiyo inatarajiwa kujitokeza katika ukanda wa Pwani ya Kaskazini mwa Bahari ya Hindi na inaweza kuathiri shughuli za kiuchumi, uvuvi pamoja na usafirishaji baharini.
Aidha, kesho Alhamisi, upepo mkali unatarajiwa kuendelea katika maeneo ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani ikiwemo visiwa vya Mafia, pamoja na Unguja na Pemba visiwani Zanzibar.
