Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam

20/5/2026 Watumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wametakiwa kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara na kufahamu “namba zao” ikiwemo shinikizo la damu, kiwango cha sukari, mafuta mwilini, mapigo ya moyo na uwiano wa uzito kwa urefu (BMI) ili kutambua mapema vihatarishi vya magonjwa yasiyoambukiza kabla hayajaleta madhara makubwa kiafya.

Wito huo umetolewa hivi karibuni na Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Monica Kaganga wakati wa zoezi la utoaji wa elimu na huduma za uchunguzi wa afya kwa watumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) jijini Dodoma kupitia kampeni ya Jua Namba Zako.

Akizungumza katika zoezi hilo Dkt. Monica alisema njia mojawapo ya kugundua mapema magonjwa yasiyoambukiza ni wananchi kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara na kufahamu viwango vya afya zao kabla hali haijawa mbaya.

“Njia mojawapo ya kutambua dalili za magonjwa haya mapema ni kujua namba zako. Tunapima shinikizo la damu, kiwango cha sukari, mafuta mwilini, mapigo ya moyo pamoja na uwiano wa uzito kwa urefu (BMI)”, alisema Dkt. Monica.

Alisema mwitikio wa watumishi wa REA umekuwa mkubwa tangu kuanza kwa zoezi hilo ambalo lilifanyika kwa muda wa siku tatu jambo linaloashiria kuongezeka kwa uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara.

“Mwitikio umekuwa wa kuridhisha na tunaamini elimu hii imewasaidia wafanyakazi kuelewa umuhimu wa kujua hali zao za afya. Tutaendelea kuimarisha kampeni ya Jua Namba Zako ili kuwafikia wananchi wengi zaidi”, alisema Dkt. Monica.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy aliishukuru JKCI kwa kupeleka huduma za elimu na uchunguzi wa afya kwa watumishi wa taasisi hiyo.

“Tunamshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge pamoja na wataalamu wake kwa kutuletea huduma hizi muhimu. Watumishi wamepima vipimo vya shinikizo la damu, sukari pamoja na huduma nyingine za uchunguzi wa afya”, alisema Mhandisi Saidy.

Alitoa rai kwa waajiri wengine kuiga utaratibu huo kwa kuwaleta wataalamu wa afya katika maeneo ya kazi ili kuwasaidia watumishi kupima afya zao mapema.

Naye Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa REA, Magdalena Muhazi alisema elimu ya jinsi ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza waliyoipata imewasaidia kuongeza uelewa kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa hayo yakiwemo ya moyo.

“Tumeelezwa mambo mengi muhimu kuhusu afya zetu ikiwemo madhara ya matumizi mabaya ya pombe, ulaji usiofaa, msongo wa mawazo na umuhimu wa kupima afya mara kwa mara”, alisema Magdalena.

Mkurugenzi wa Umeme Vijijini wa REA, Mhandisi Jones Olotu alisema huduma hiyo imewapa fursa watumishi kujua hali zao za afya mapema pamoja na kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu mazoezi na mtindo bora wa maisha.

“Tumepata fursa ya kufahamu hali za afya zetu kupitia kampeni ya Jua Namba Zako. Mbali na vipimo pia tumepata ushauri wa kitaalamu kuhusu umuhimu wa kufanya mazoezi na kuishi maisha yenye mtindo unaolinda afya zetu”, alisema Mhandisi Olotu.

Kampeni ya Jua Namba Zako inaendelea kuwa chachu ya kuhamasisha wananchi kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kubaini mapema vihatarishi vya magonjwa yasiyoambukiza kupitia elimu na vipimo vinavyotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).