Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amepongeza jitihada zinazofanywa na sekta ya ushirika kwa kuhakikisha Mkoa unaendelea kuwa kinara wa maendeleo ya ushirika nchini.

Amesema mafanikio yanayopatikana kupitia vyama vya ushirika yameendelea kuupa mkoa heshima kubwa kitaifa kutokana na tuzo mbalimbali zinazotokana na utendaji mzuri wa vyama hivyo.

Kunenge ameeleza hayo katika Kikao cha Jukwaa la Sita la Ushirika Mkoa wa Pwani kilichofanyika katika Ukumbi wa Density, Kibaha, kikihusisha viongozi, wanachama wa vyama vya ushirika pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo ya ushirika kutoka ndani na nje ya mkoa huo.

Aidha, Kunenge amewataka viongozi wa vyama vya ushirika kupunguza gharama za uendeshaji ili huduma zinazotolewa kwa wanachama ziwe nafuu zaidi na zenye manufaa kwa wananchi.

Amesisitiza umuhimu wa kuzingatia uwazi, uwajibikaji na maadili katika usimamizi wa vyama vya ushirika.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Ushirika Mkoa wa Pwani, Charles Maguye amefafanua, kupitia jitihada za Serikali chini ya Samia Suluhu Hassan, Mkoa huo umeendelea kupata mafanikio katika sekta ya ushirika ikiwemo ongezeko la hisa na akiba za SACCOS, utoaji wa mafunzo kwa viongozi na wanachama pamoja na vyama vya ushirika kupata tuzo mbalimbali za kitaifa.

Amebainisha licha ya mafanikio wanakabiliwa na changamoto ya ubovu wa barabara, ucheleweshaji wa malipo kwa baadhi ya SACCOS na masoko ya mazao, huku wanaushirika wakiiomba serikali kuendelea kushirikiana nao katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo.