Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea tani 25 za tende kutoka kwa Ufalme wa Saudi Arabia ikiwa ni utamaduni endelevu unaoonesha mshikamano wa kihistoria na kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.

Mapokezi hayo yamefanyika Mei 19, 2026 kwenye Ofisi ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya tende hizo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe (Mb.) ametoa shukrani za dhati kwa niaba ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na wananchi wa Tanzania na kupongeza utamaduni huo endelevu unaofanyika kila mwaka kupitia Kituo cha Msaada wa Kibinadamu cha King Salman bin Abdulaziz Al Saud.

Aidha, amesisitiza kuwa mbali na zawadi za tende, Serikali ya Tanzania inaishukuru Saudi Arabia kwa misaada matibabu hususan upasuaji wa hivi karibuni uliofanikiwa wa kuwatenganisha pacha wa Kitanzania walioungana: Nancy na Nice Anjelina Magore George, uliofanyika katika Kituo cha Matibabu cha King Abdulaziz jijini Riyadh chini ya maelekezo ya Serikali ya Saudi Arabia.

Naibu Waziri Maghembe ameupongeza pia Ufalme huo kwa ufadhili wa masomo, programu za kujenga uwezo wa kiutendaji, na kuunga mkono Tuzo ya Kila Mwaka ya Kimataifa ya Quran Tukufu ya Tanzania (TIHQA) zinazotolewa na serikali hiyo.

Kwa upande wake, Balozi wa Ufalme wa Saudi Arabia nchini Tanzania Mhe.Yahya Ahmed bin Okeish, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wanaouonesha siku zote.

Alieleza kuwa kwa mwaka 2026 jumla ya tani 80 za tende kutoka Saudi Arabia zimeingizwa nchini ikijumuisha tani 25 kwa ajili ya Tanzania Bara, tani 30 zilizosambazwa wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, na 25 zilizotengwa kwa ajili ya Zanzibar.