NA FAUZIA MUSSA
MKUU wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Moh’d Ali Abdalla amesema mfumo wa taarifa za maafa wa Zanzibar (ZDMIS) utakuwa mkombozi mkubwa kwa jamii katika kusaidia kupunguza na kuondosha changamoto zinazotokana na majanga mbalimbali.
Akizungumza katika kikao cha kuthibitisha mapitio ya mfumo huo kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Tume ya Uchaguzi Maisara, alisema matumizi ya teknolojia katika sekta ya maafa ni hatua muhimu ya kuimarisha usalama wa wananchi pamoja na kuongeza ufanisi wa utoaji wa taarifa za tahadhari.
Alisema kabla ya kuanzishwa kwa mfumo huo, jamii ilikuwa ikikabiliana na changamoto nyingi za majanga kwa kutokuwa na mfumo madhubuti wa kupata taarifa sahihi na kwa wakati, hali iliyosababisha athari mbalimbali kwa wananchi na mali zao.
“Uwepo wa mfumo huu utasaidia jamii kujikinga na majanga tofauti kwa kupata taarifa kwa wakati pamoja na kuelekezwa namna ya kuchukua tahadhari mapema,” alisema.
Aidha alisema maendeleo ya sayansi na teknolojia duniani yanaendelea kwa kasi kubwa, hivyo kuna umuhimu wa kuhakikisha mfumo huo unaendana na mabadiliko hayo ili usipitwe na wakati.
“Mfumo huu unahitaji kuwekwa katika misingi imara ili uweze kudumu kwa muda mrefu na kuepusha serikali kuingia tena katika gharama kubwa za kuunda mfumo mwingine hapo baadaye,” aliongeza.
Sambamba na hayo, Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka wataalamu wazalendo waliobuni mfumo huo kuhakikisha unawekewa ulinzi madhubuti wa kimtandao ili kuzuia kuingiliwa na mifumo mingine ambayo inaweza kusababisha athari au upotevu wa taarifa muhimu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar, Makame Khatib Makame alisema mfumo huo ni wa shirikishi kwani unawakutanisha wadau mbalimbali wenye jukumu la kutoa taarifa na maoni yatakayosaidia kuimarisha zaidi.
Alisema mfumo huo utajumuisha masuala ya elimu kwa umma, tahadhari za majanga, mawasiliano pamoja na utoaji wa taarifa za matukio mbalimbali, huku sekta zote zikipewa nafasi ya kuingiza taarifa zinazohusu taasisi zao.
Naye Ofisa wa Maji na Usafi wa Mazingira wa UNICEF Zanzibar, Marko Msambazi alisema shirika hilo lina imani kuwa kukamilika kwa mfumo huo kutasaidia upatikanaji wa taarifa sahihi za maafa pamoja na kuimarisha hatua za kinga katika jamii.
Alisema UNICEF itaendelea kushirikiana na Serikali ya Zanzibar katika kuimarisha mifumo ya usalama na huduma za kijamii, akibainisha kuwa mfumo huo utakuwa na mchango mkubwa katika kuwalinda watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi wakati wa majanga.

