Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mhe. Lucy Edward Mwakyembe, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kulipa madeni ya wakandarasi na wazabuni, bungeni jijini Dodoma. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)
………

Na. Jordan Mbwambo, WF, Dodoma.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) amesema kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kuendelea kulipa madeni ya wakandarasi, wazabuni, na watumishi nchini ili kulinda mitaji yao na kudhibiti ongezeko la madeni mapya.

Hayo yamebainishwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mhe. Lucy Edward Mwakyembe, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kulipa madeni ya wakandarasi na wazabuni.

Mhe. Munde alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha imekuwa ikitenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya kugharamia ulipaji wa madeni ya wakandarasi, wazabuni na watumishi.

‘‘Katika mwaka 2025/26, shilingi bilioni 700 zilitengwa ambapo, hadi Februari 2026, jumla ya shilingi bilioni 477.6 zimetolewa, pia Serikali imetenga shilingi bilioni 800 katika mwaka wa fedha 2026/27 kwa ajili ya kugharamia ulipaji wa madeni yaliyohakikiwa’’, alisema Mhe. Munde.

Aidha, Mhe. Munde alifafanua kuwa katika kuhakikisha kuwa suala la madeni ya wakandarasi na wazabuni linadhibitiwa, Serikali imeendelea kutoa maelekezo kwa Maafisa Masuuli kupitia Waraka mbalimbali za utekelezaji wa bajeti na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti katika mwaka husika.

Mhe. Munde aliongeza kuwa Serikali imeendelea kutoa maelekezo kwa Mafungu kutenga bajeti kwa ajili ya ulipaji wa madeni ya wakandarasi, wazabuni na watumishi.

Aidha, Serikali imeelekeza Maafisa Masuuli kutumia mifumo ya kudhibiti matumizi pamoja na kuhakikisha kuwa mchakato wowote wa ununuzi unaanzishwa baada ya kujiridhisha uwepo wa bajeti na uhakika wa upatikanaji wa fedha.