Na John Bukuku, Dar es Salaam

Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imezitaka kampuni zinazotoa huduma katika masoko ya mitaji nchini kuendelea kubuni bidhaa mpya za kifedha zitakazopanua fursa za uwekezaji kwa wananchi wa ndani na wa kimataifa pamoja na kusaidia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo na biashara.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Utafiti, Sera na Mipango wa CMSA, Alfred Mkombo, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama, wakati wa uzinduzi wa Programu ya Hatifungani ya Muda wa Kati (MTN Programme) ya Kampuni ya iTrust Finance Limited yenye thamani ya Shilingi bilioni 100 uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Mkombo amesema CMSA itaendelea kusimamia utekelezaji wa mikakati mbalimbali inayolenga kukuza maendeleo ya masoko ya mitaji nchini kwa lengo la kujenga uchumi wenye ushindani na kuleta maendeleo kwa wananchi.

“Napenda kutoa wito kwa kampuni zenye leseni ya kutoa huduma katika masoko ya mitaji kuendeleza mikakati ya kuanzisha bidhaa bunifu zinazopanua na kuongeza fursa kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa,” amesema Mkombo.

Katika hatua hiyo, Kampuni ya iTrust Finance Limited imezindua rasmi hatifungani yake ijulikanayo kama iTrust Bond, ikiwa ni hatifungani ya kwanza nchini kutolewa na kampuni wakala wa soko la hisa na msimamizi wa mifuko ya uwekezaji Tanzania.

Kwa mujibu wa kampuni hiyo, awamu ya kwanza ya programu hiyo inalenga kukusanya Shilingi bilioni 15 pamoja na nyongeza ya Shilingi bilioni 5 kupitia chaguo la ziada, huku wawekezaji wakitarajiwa kupata riba ya asilimia 13 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka minne.

Imeelezwa kuwa riba ya hatifungani hiyo italipwa kila baada ya miezi mitatu bila kukatwa kodi ya zuio (withholding tax), hatua inayolenga kuwapa wawekezaji mapato ya uhakika na yanayotabirika.

Hatifungani hiyo iliyopata idhini ya CMSA ilifunguliwa rasmi Mei 18, 2026 na itafungwa Juni 12, 2026, huku ikitarajiwa kuorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ili kuwezesha biashara katika soko la upili.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa iTrust Finance Limited, Bw. Faiz Arab, alisema kampuni hiyo imeweka kiwango cha chini cha uwekezaji kuwa Shilingi 500,000 ili kutoa nafasi kwa wawekezaji binafsi na taasisi kushiriki kwa urahisi zaidi.

Amesema fedha zitakazopatikana kupitia hatifungani hiyo zitatumika kuongeza uwezo wa utoaji wa mikopo, kuwekeza katika majukwaa ya kidijitali ya kisasa pamoja na kuimarisha mtaji wa uendeshaji wa kampuni.

Katika hatua nyingine, Faiz Arab alizindua programu ya simu ya iTrust App ambayo itawawezesha watumiaji kuwekeza katika hatifungani, hisa na mifuko ya uwekezaji huku wakifuatilia uwekezaji wao katika sehemu moja.

iTrust Finance Limited ni taasisi ya huduma za kifedha ya daraja la pili (Tier 2) inayosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pamoja na CMSA, huku ikitoa huduma za uwakala wa soko la hisa, ushauri wa uwekezaji, usimamizi wa mifuko ya uwekezaji pamoja na mikopo ya kawaida na inayozingatia misingi ya Shariah kupitia kitengo chake cha Imaan Finance.