Jeshi Polisi mkoani Arusha limesema kwa kipindi cha kuanzia Aprili 18, 2026 hadi sasa, watuhumiwa 176 wamehukumiwa vifungo mbalimbali kwa makosa ulawiti, ubakaji, wizi, dawa za kulevya, kujeruhi, uvunjaji, kupatikana na nyara za serikali na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu baada ya kufikishwa Mahakamani. 

Akitoa taarifa hiyo leo Mei 18, 2026 Kamanda wa Polisi Mkoani humo, SACP Justine Masejo amesema kati ya waliohukumiwa kwa makosa makubwa, mtuhumiwa 01 alihukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kosa la mauaji huku mtuhumiwa 01 akihukumiwa kifungo cha maisha gerezani kwa kosa la kulawiti, 

Ameendelea kufafanua kuwa watuhumiwa 02 walihukumiwa miaka 30 gerezani kwa makosa ya kubaka na wizi na watuhumiwa wengine 02 walihukumiwa miaka 20 gerezani kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kupatikana na nyara za serikali. 

Aidha, amebainisha kuwa kupitia operesheni dhidi ya dawa za kulevya, walifanikiwa kukamata watuhumiwa 19 wakiwa na Mirungi Kilogramu 90 na watuhumiwa 12 wakiwa na bhangi misokoto 177. 

Pia kwa kipindi hicho walifanikiwa kukamata Watuhumiwa 33 wakiwa na Pombe ya moshi lita 434 na mitambo 09 ya kutengeneza pombe hiyo.

SACP Masejo amesema operesheni hizo zinaendelea kufanyika maeneo yote katika mkoa huo, ambapo amewataka baadhi ya watu wachache wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu kuacha mara moja vitendo hivyo kwani watawakamata na kuchukua hatua za kisheria dhidi yao. 

Sambamba na hilo, wataendelea kuchukua hatua kwa madereva wachache wanaoendesha vyombo vya moto kwa kutofuata sheria za usalama barabarani hususani mwendokasi, ulevi na kupita magari mengine bila kuchukua tahadhari. 

Jeshi la Polisi mkoani humo limewapongeza wananchi wote wanaotoa taarifa za uhalifu na wahalifu katika maeneo yao hususani katika kipindi hiki kuelekea msimu mkubwa wa utalii katika Mkoa huo.