Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera amesema kuwa Serikali inaendelea kufanya maboresho mbalimbali ili kuleta mageuzi katika Sekta ya Sheria nchini, Mhe. Dkt. Homera ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo maalumu kwa Mawakili wa Serikali yaliyoandaliwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, yanayofanyika Jijini Arusha, tarehe 18 Mei, 2026.

Akizungumza wakati akifungua mafunzo kwa Mawakili wa Serikali Dkt. Homera amesema kuwa kupitia mafunzo hayo, Mawakili wa Serikali watapata fursa ya kujengewa uwezo katika maeneo ya kimkakati yakiwemo usimamizi wa mikataba ya ujenzi na manunuzi, Sheria za Anga na utatuzi wa migogoro ya anga, Sheria za kodi katika sekta ya Mafuta na Gesi, uendeshaji wa mashauri ya kodi, na Uendeshaji wa Mashauri katika Mabaraza mbalimbali ya Utoaji Haki. 

*”Mada hizi ni mahsusi kabisa katika kufikia lengo la Wizara ya Katiba na Sheria na taasisi zake la maono ya Mageuzi katika Sekta ya Sheria.”* Amesema Dkt. Homera 

Aidha, Waziri wa Katiba na Sheria ameeleza umuhimu wa maboresho mbalimbali ya Kisheria kwakuwa Sheria ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa Dira ya 2050, ambapo amesema kuwa pamoja na mambo mengine taifa linahitaji watu imara katika kusimamia sheria zitakazoleta amani, utulivu, maendeleo ya kiuchumi kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Vilevile, Dkt. Homera amesema kuwa kuptia mafunzo haya Mawakili wa Serikali wataweza kushauri ipasavyo, kusimamia vizuri mashauri ya Serikali na kuwezesha Serikali Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufikia malengo yake ya DIRA 2050.

*”Kama mnavyofahamu kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 imeweka misingi yake katika sekta ya sheria ambayo ni Utawala, Amani, Usalama na Utulivu”.* Amesema Waziri wa Katiba na Sheria

Katika hatua nyingine, Dkt. Homera amewasisitiza Mawakili wa Serikali kufuatilia mafunzo hayo kwa utulivu kwani mada hizo zimegusa maeneo muhimu sana katika utekelezaji wa majukumu ya Mawakili wa Serikali.