Na. Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma

Serikali Kupitia Wizara ya ujenzi imesaini mkataba wa upanuzi wa barabara ya Dodoma Mjini hadi Chamwino Ikulu yenye urefu wa kilometa 32 kuwa ya njia sita, mradi utakaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 241 hadi kukamilika kwake mkataba huo umesainiwa na  TANROADS kwa niaba ya Serikali na China Railway Construction Engineering Group (CRCEG) ya China, kwa lengo la kutekeleza upanuzi wa barabara hiyo kuwa ya njia sita.Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, amesema kuwa mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuendelea kuboresha miundombinu ya usafiri na kuifanya Dodoma kuwa jiji la kisasa linalovutia wawekezaji na wananchi.

Hafla ya utiani saini mkataba  imefanyika Mei 18,2026 Jijini Dodoma 

Aidha, Waziri Ulega amebainisha kuwa Serikali imeelekeza uwepo wa taa za kisasa, bustani pamoja na njia salama za watembea kwa miguu ili kuongeza usalama na mvuto wa barabara hiyo hususan nyakati za usiku.Pia ameongeza kuwa TANROADS inapaswa kuhakikisha mkandarasi anasimamiwa ipasavyo ili mradi huo ukamilike kwa ubora unaotakiwa na ndani ya muda uliopangwa.Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mohamed Besta, amesema kuwa mradi huo utatekelezwa kwa mfumo wa Sanifu na Jenga (Design and Build) na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 36.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Seleman Kakoso, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo inayochochea ukuaji wa uchumi na kuboresha huduma za usafiri nchini.