Na.Sophia kingimali.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka wafanyabiashara kuacha tabia ya kutumia vipimo batili akisema wanaowaibia wananchi kupitia mizani zisizo sahihi ni sawa na vibaka wengine wanaopaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumza leo Mei 18,2026 katika maadhimisho ya kuelekea Siku ya Vipimo Duniani yaliyofanyika katika soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam, Chalamila amesema matumizi ya vipimo sahihi ni msingi wa haki, uaminifu na ustawi wa biashara nchini.

Ameongeza kuwa wananchi wanapokwenda sokoni kununua bidhaa mbalimbali wanatarajia kupata kiwango halisi cha bidhaa walizolipia na si kupunjwa kwa kutumia mizani zisizo sahihi.

“Anayepunguza vipimo kwa makusudi ni mwizi kama walivyo wezi wengine, kwa sababu anachukua fedha za wananchi bila kutoa thamani halisi ya bidhaa,” amesema Chalamila.

Aidha, amewataka watendaji wa Wakala wa Vipimo nchini kuendelea kuwa wakali dhidi ya wafanyabiashara wanaotumia mizani bandia huku akisisitiza kuwa matumizi ya vipimo sahihi hujenga imani kati ya muuzaji na mnunuzi.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka viongozi wa serikali kuhakikisha wanawatumikia wananchi kwa haki na uwazi akisema viongozi wanapaswa kuwa tayari kubeba changamoto zinazowakabili wananchi wao.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Ilala, Muhono Nashoni, amesema wamegawa mizani katika masoko mbalimbali ya Dar es Salaam ili kuhamasisha matumizi ya vipimo sahihi hasa katika soko la Kariakoo ambalo ni kitovu cha biashara nchini.

Amesema soko la Kisutu limetunukiwa tuzo kwa kuongoza kwa matumizi sahihi ya vipimo huku akieleza kuwa hatua hiyo itakuwa chachu kwa masoko mengine kuiga mfano huo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema uwepo wa vipimo sahihi ni ishara ya haki katika biashara na utekelezaji wa maono ya serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa usawa.

Maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani huadhimishwa kila mwaka Mei 20 ambapo mwaka huu kitaifa yatafanyika mkoani Dodoma huku kauli mbiu ikisisitiza kujenga imani katika utekelezaji wa sera kupitia matumizi sahihi ya vipimo.